Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa pamoja wamekamilisha ujenzi wa Mradi mkubwa na wa kimkakati wa Kusambaza Gesi Asilia katika maeneo yaliyopitiwa na mkuza wa bomba la gesi katika mikoa ya Lindi na Pwani ambapo REA imefadhili na TPDC imejenga na kusambaza miundombinu hadi kwa mtumiaji wa mwisho (Mwananchi) ambapo hadi Mradi umekamilika, REA imetumia jumla ya shilingi bilioni 6.8 kugharamia Mradi huo.
Akizungumza na Wanahabari maara baada ya kuisha kwa zoezi la ukaguzi wa miundombinu ya Mradi huo eneo la Kisemvule mkoani Pwani, tarehe 22 Januari, 2026 (Alasiri) Mhandisi Emanuel Yesaya, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, amesema jumla ya kaya 530 tayari zimefikishiwa miundombinu ya Mradi huo, na kuongeza kuwa Mradi umetekelezwa kwa kusambaza mabomba ya gesi asilia ya ukubwa mbalimbali yenye urefu wa jumla ya kilomita 25 pamoja na kituo kidogo cha kupunguza mgandamizo wa gesi katika mkoa wa Pwani ambapo miundombinu ya kusambaza gesi asilia imefika hadi majumbani katika kata ya Vikindu, kijiji cha Kisemvule.
Mhandisi, Yesaya amesema miundombinu ya gesi asilia imesambazwa hadi kwenye nyumba za Wananchi walio katika wigo wa Mradi na kuongeza kuwa Wananchi wapo huru kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia ambapo itawalazimu kununua majiko ya gesi ili kuanza kufurahia matumizi ya gesi asilia.
“Mfumo wa gesi uliowekwa unamwezesha Mwananchi kununua gesi wakati wowote kupitia namba maalum ya malipo ya Serikali (Control number).” Amekaririwa, Mhandisi, Yesaya.
Aidha ametoa wito kwa Wananchi kutumia gesi asilia kwani ni nafuu akisisitiza kuwa matumizi ya nishati hiyo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, amesema REA kwa kushirikiana na TPDC itaendelea kutoa elimu kwa Wananchi ili kuwawezesha kuelewa umuhimu wa kutumia nishati safi, hususan gesi asilia, kwa ajili ya kupikia.
#kilichoborakabisa
(Feed generated with FetchRSS)