
Sudan ni “inakabiliwa na mambo mabaya zaidi ambayo yametokea duniani,” Waziri wa Masuala ya Jamii wa Sudan amewaambia wenzetu wa shirika la habari la Agence France-Presse (AFP). Kulingana na Sulaima Ishaq al-Khalifa, wanawake ndio waathiriwa wakuu wa mzozo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, ambao umeendelea tangu mwezi Aprili 2023. Ameelezea ubakaji, utumwa wa kingono, na ndoa za kulazimishwa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Hakuna kikomo cha umri,” ameelezea Sulaima Ishaq al-Khalifa. Ubakaji unaweza kuwalenga wanawake wa rika zote, kuanzia wazee hadi watoto, na unaweza kufanywa “mbele ya familia,” kulingana na Waziri wa Masuala ya Jamii wa Sudan. Mwanasaikolojia huyu, mwanaharakati dhidi ya ukatili unaofanyiwa wanawake, hivi karibuni alijiunga na serikali inayounga mkono jeshi.
Kulingana na data ya wizara, zaidi ya visa 1,800 vya ubakaji vimerekodiwa tangu kuanza kwa vita nchini Sudan mnamo mwezi Aprili 2023. Takwimu hizi hazijumuishi ukatili uliofanywa Darfur na Kordofan kuanzia mwisho wa mwezi Oktoba 2025. Lengo, kulingana na waziri, ni kudhalilisha, kuwalazimisha watu kuondoka majumbani mwao, na kuharibu mfumo wa kijamii. Ubakaji mkubwa umerekodiwa. Waathiriwa wamegeuzwa kuwa watumwa wa ngono, wengine wakiuzwa na mitandao ya biashara haramu.
Waathiriwa washindwa kujieleza
Unyanyasaji wa kijinsia upo pande zote mbili, anafafanua zaidi, lakini anauelezea kama “wa kimfumo” na unaotumika kama silaha ya vita na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wanaopigana na jeshi.
Moja ya matatizo, anakiri, ni kuwafanya waathiriwa wazungumze. Baadhi ya familia hupendelea kuwalazimisha binti zao kuolewa ili kuficha kilichotokea.