MARA: Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea kutoa wito kwa Watanzania na wawekezaji kwa ujumla kuwekeza katika sekta ya uvuvi, hususan uvuvi wa vizimba (cage fish farming) katika Mkoa wa Mara kupitia vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi vilivyowekwa na Serikali.

Wito huo umetolewa Januari 24, 2026 wakati wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Uwekezaji wa Ndani inayotekelezwa na mamalaka, ambapo timu ya mamlaka hiyo ilifanya ziara ya kutembelea miradi ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba mkoani Mara.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji, TISEZA, George Mukono alisema Serikali imeweka vivutio mahsusi vya uwekezaji katika sekta ya uvuvi, ikiwemo msamaha wa ushuru wa forodha kwa asilimia 100 kwa wawekezaji wanaoagiza rasilimali za mtaji (capital goods) kwa matumizi ya moja kwa moja katika shughuli za uvuvi wa vizimba.

Alifafanua kuwa miongoni mwa vifaa vinavyonufaika na msamaha huo ni pamoja Vifaa vya kuelea (floats) vya nyavu za uvuvi, Nyavu za uvuvi ikiwemo boti au vyombo vya kusafiria kwenda vizimbani na kusafirisha samaki kutoka vizimbani hadi forodhani, Kamba za nailoni za uvuvi (nylon fishing twine), injini za nje (outboard engines), Ndoano na nyuzi za uvuvi.

Kwa mujibu wa TISEZA, vivutio hivi ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukuza na kuvutia uwekezaji katika sekta ya uvuvi, kwa lengo la kukuza uchumi, kuongeza ajira hususan kwa vijana, kuinua pato la taifa, na kuimarisha usalama wa chakula.Aidha, hatua hizi zinalenga kupunguza uagizaji wa zana za uvuvi kutoka nje na kuchochea uzalishaji wa ndani, hali inayothibitisha kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wawekezaji kupitia unafuu wa mtaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *