,

Waandishi wa
habari nchini Tanzania wamezuiwa kuhudhuria vikao vya Tume ya Rais ya
Uchunguzi, huku wahanga wa machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 2025 wakitoa
ushuhuda.

Tume hiyo
iliyoundwa na Rais Samia Suluhu, inachunguza vurugu hizo kwa lengo la kubaini
sababu zake na kupendekeza njia za kuendeleza maridhiano ya kitaifa.

Vikao vya awali
vilikuwa wazi kwa vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa kuripoti juu ya ushuhuda wa waathiriwa.

Hata hivyo,
wanahabari na baadhi ya vyombo vya habari vilisema hawakuruhusiwa kuhudhuria
vikao vya ufuatiliaji siku ya Jumamosi.

Siku ya Ijumaa waathiriwa walitoa maelezo ya kina kuhusu ghasia za siku ya
uchaguzi.

Taarifa
iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na gazeti la The Citizen
ilisema wanahabari waliruhusiwa kuripoti vikao vya Ijumaa, ambapo waathiriwa
walitoa ushuhuda wao.

Hapo jana Mwananchi liliandika: “Leo Januari
24, 2026 tume ilikutana katika Wilaya ya Ubungo. Tofauti na vikao vya awali,
waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia ukumbini wakati wa kutoa
ushahidi.”

Profesa Ibrahim
Juma, anayeongoza uchunguzi huo aliwaambia waliohudhuria Jumamosi kuwa
waandishi wa habari hawataruhusiwa wakati wa kutoa ushahidi. Alisema uamuzi huo
ulifanywa ili kulinda faragha ya mashahidi.

Wakazi walitoa
maelezo ya matukio waliyoshuhudia au uzoefu siku ya uchaguzi, wakielezea athari
za kibinafsi za machafuko hayo.

Kutengwa kwa
waandishi wa habari kunaashiria mabadiliko katika mbinu ya uchunguzi na kumezua
maswali kuhusu uwazi.

Mwandishi wa
habari wa ndani aliiambia BBC kwamba uamuzi huo unatia wasiwasi.

“Inasikitisha
kwamba waandishi wa habari wananyimwa nafasi ya kuripoti. Baadhi ya shuhuda
hizi tayari zimetolewa. Wanajaribu kuficha nini? … Je, hii ni kwa sababu ya
habari za hivi majuzi? au amri kutoka kwa mamlaka? Tunaheshimu faragha, lakini
si kila shahidi ameomba faragha juu ya ushuhuda wao,” mwandishi wa habari
alisema.

Bado haijabainika
ikiwa wanahabari wataruhusiwa kuhudhuria vikao vijavyo vya tume hiyo.

Pia unaweza kusoma:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *