Katika kile kinachoitwa ushindi wa biashara huria, EU na India zimejiandaa kukubaliana kuhusu “mama wa mikataba yote” na makubaliano ya ulinzi yanayolenga kuivutia India kutoka kwa uhusiano wake wa karibu wa kisiasa na kijeshi na Urusi.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Na: RFI na mashirika mengine

Matangazo ya kibiashara

Ingawa Marekani imesema ushuru mkubwa unakusudiwa kuizuia India kununua mafuta ghafi ya Urusi, inaonekana EU imechukua mbinu tofauti ya kuivutia India kutoka kwenye mzunguko wa Moscow – biashara zaidi na uhusiano imara wa ulinzi.

Katika mkutano wa kilele mjini New Delhi wiki hii, EU na India zinatarajiwa kukamilisha makubaliano ya biashara huria na kusaini ushirikiano mpya wa usalama na ulinzi, makubaliano ya tatu kati ya EU na nchi ya Asia baada ya Japan na Korea Kusini.

“Licha ya hoja za muda mrefu za kupendelea ushirikiano wa karibu, ikiwa ni pamoja na ushindani wa pamoja na China na motisha za biashara kwa pande zote mbili, ilikuwa ni uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na ushuru wa adhabu wa Trump ambao umeleta kasi katika uhusiano huo,” amesema Praveen Donthi, mchambuzi mkuu katika shirika linalohusika na kutatua migogoro la International Crisis group (ICG) lenye makao yake makuu Delhi.

EU, India zachonga njia kabambe

Kabla ya mkutano huo, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa watakuwa wageni wakuu katika sherehe za Siku ya Jamhuri ya India leo Jumatatu, wakati ndege mbalimbali kutoka kote nchini zitaonyeshwa pamoja na vifaru na wanajeshi wakifanya guaride kubwa. Ursula von der Leyen na Antonio Costa ni maafisa wa kwanza wakuu wa EU kualikwa kushiriki katika tukio hilo.

Siku ya Jumanne, maafisa wanatarajiwa kuhitimisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya biashara ambayo yataunda soko la karibu watu bilioni 2 ambao wanachangia robo ya Pato la Taifa la dunia. Von der Leyen na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia watahudhuria Kongamano la kwanza la Biashara kati ya EU na India, pamoja na zaidi ya wafanyabiashara wakubwa ishirini na wanne kutoka pande zote mbili.

EU na India pia zinatarajiwa kuzindua mfumo mpya wa ushirikiano kuhusu uhamaji wa wafanyakazi, ambapo EU inatarajia kuvutia wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu na wa msimu kutoka India. “Bila shaka, sambamba na kile soko la ajira katika Umoja wa Ulaya linahitaji,” afisa mmoja wa EU amesema, kwa sharti la kutotajwa jina.

Kwa kuongezea, EU inatarajia kuchunguza jukumu linalowezekana kwa India katika mpango mkuu wa utafiti na uvumbuzi wa EU, Horizon.

“Viongozi pia watagusia muunganisho,” afisa huyo ameongeza. “Tunalenga hasa Ukanda wa Kiuchumi wa India-Mashariki ya Kati-Ulaya, IMEC, ambao ungeunda miunganisho mipya ya usafiri, kidijitali na nishati kati ya India na Ulaya” kupitia nchi za Kiarabu na Israel.

EU, India zinatarajia kupata nini?

“Ulaya inataka kufanya biashara na vituo vya ukuaji vya leo na nguvu za kiuchumi za karne hii,” von der Leyen alisema siku ya Jumatano katika Jukwaa la Uchumi wa Dunia huko Davos, akiita makubaliano ya biashara na India “mama wa mikataba yote.”

Kulingana na data ya EU, EU ni mshirika mkubwa wa biashara wa India; biashara ya bidhaa ilifikia thamani ya euro Bilioni 120 mwaka 2024, 11.5% ya biashara yote ya India. Kufikia mwaka 2030, India inakadiriwa kuwa nchi ya tatu yenye uchumi mkubwa duniani baada ya China na Marekani.

EU inatumai India itapunguza ushuru wake maarufu wa juu kwa magari yanayoagizwa kutoka nje, ambayo kwa sasa ni zaidi ya 100%, na kuongeza sekta ya magari ya Ulaya licha ya ushindani kutoka China. Na, huku Wahindi wakipanda ngazi katika uhamaji wa kiuchumi, tasnia ya pombe barani Ulaya iko tayari kuzima kiu yao ya mvinyo na pombe kali. Chini ya makubaliano ya biashara, India inatarajiwa kuondoa ushuru wake wa juu sana kwa pombe – hadi 150% kwa mvinyo zinazoagizwa kutoka nje.

Mwaka jana, chini ya makubaliano yake ya biashara huria na Uingereza, India ilikubali kupunguza ushuru kwa magari na pombe lakini kwa awamu – ili kupunguza athari kwa wazalishaji wa ndani.

Kwa upande wake, India imedai viwango rahisi vya mauzo yake ya dawa, na ufikiaji sawa wa nguo bila ushuru ambao EU inawapa majirani wa Asia kama Pakistan na Bangladesh. Delhi inatumai hii itapunguza athari za ushuru wa Marekani, ambao umekuwa ukiharibu sana sekta ya nguo ya India.

India pia inatarajia kutuma wataalamu zaidi kwa EU kwa fursa za ajira, na inatafuta ahadi za uzalishaji wa pamoja katika tasnia ya ulinzi.

Lisa Musiol, mkuu wa masuala ya EU katika shirika linalohusika na kutatua migogoro la International Crisis group (ICG) huko Brussels, amesema India ndiyo nchi ya kwanza kuchukua hatua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *