Miti milioni 691 yapandwa kampeni ya upandaji mitiMiti milioni 691 yapandwa kampeni ya upandaji miti

TANZANIA imepanda na kustawisha miti 691,523,763 katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020-2024 kupitia kampeni ya upandaji miti nchini.

Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Hifadhi ya Bayoanuai) Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Deogratius Paul amesema hayo wakati akizungumza na HabariLEO kuhusu hali ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini kama sehemu ya maadhimisho ya 27 ya kijani chini ya kaulimbiu ‘Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti’.

Amesema katika utekelezaji wa kampeni hiyo, wadau walishirikishwa kuhamasisha utekelezaji wa kampeni za ukuzaji na utunzaji wa miti kwa lengo la kupanda miti ili kuondokana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi. Amesema mafanikio hayo yanatokana na kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka kila halmashauri nchini.

Aidha, Dk Deogratius amesema Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wizara za kisekta na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inaendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi na sekta binafsi katika kampeni ya upandaji na utunzaji miti milioni 1.5 kila mwaka kwa halmashauri zote nchini.

Kuhusu kampeni ya kukijanisha Dodoma, alisema ili kuhakikisha azma hii inafikiwa, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau jijini Dodoma imeratibu utekelezaji wa kampeni ya upandaji miti mkoani humo katika msimu wa mvua ili kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoizindua Desemba 5, 2017 wakati huo akiwa Makamu wa Rais.

Dk Deogratius amesema katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na TFS imeratibu zoezi la kurudishia miti iliyoshindwa kustawi vizuri katika eneo la wazi lililopo katika Mji wa Serikali wa Mtumba. Amesema katika zoezi hilo jumla ya miti 683 itapandwa Jumanne, Januari 27, 2026 kama sehemu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Rais Samia huku zaidi ya miti 986 tayari imestawi vizuri katika eneo hilo.

Kwa upande wa usimamizi, uendelezaji mashamba ya miti ya serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk Zainabu Bungwa amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, wakala umepanda miti eneo la mashamba lenye ukubwa wa hekta 40,184 kwa ajili ya kuzalisha rasilimali za viwanda.

Aidha, Dk Zainabu amesema TFS imeanzisha mashamba mapya ya Geita, Rwamgasa, Makere na Mpepo yenye ukubwa wa hekta 143,426 katika Wilaya ya Tunduru, Kasulu na Geita huku tani 115.9 za mbegu na miche 167,045,880 ikioteshwa. Sambamba na hayo, Dk Zainabu alisema wakala una utaratibu wa kugawa miti kwa wadau nchi nzima ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwenye shule na wananchi nchini pamoja na kuratibu halimashauri kwa kuwezesha upandaji wa miti.

Kampeni za upandaji miti zinahimiza mti wa leo ni maisha ya kesho, ni mvua ya kesho, ni maji ya kesho na ni ardhi salama ya kesho. anza sasa, mhimize na mwingine. SOMA : Samia ataja mambo 3 ulinzi mazingira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *