WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imepokea Sh bilioni 10.5 kwa ajili ya kutoa mikopo ya masharti nafuu na imeshatoa Sh bilioni 1.3 kwa wafanyabiashara 588. Pia, imesema serikali imesajili wafanyabiashara ndogondogo 119,595 kupitia mfumo wa usimamizi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo (WBMMIS).
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani katika Serikali ya Awamu ya Sita kipindi cha pili. “Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Sh milioni 337.9 zimetolewa kwa wanawake 45 kwa riba nafuu ya asilimia 4 huu ni mfuko mdogo ulipo wizarani unawakopesha wafanyabiashara waliosajiliwa,” alisema Dk Gwajima jijini Dodoma.
Amesema kupitia WBMMIS wafanyabiashara ndogondogo wanawake 73,341, wanaume 46,254, machinga 103,102 babalishe na mamalishe 12,384 na waendesha bodaboda na bajaji 4,109 wamerasimishwa. Pia, Dk Gwajima amesema kupitia mfumo wa Wezesha Portal uliopo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) vikundi 6,041 vya wajasiriamali vimetambuliwa na kusajiliwa vikiwemo vya wanawake 3,207 vijana 2,318 walemavu 516 na kufanya wafanyabiashara 30,205 kusajiliwa.
Amesema kupitia mfumo wa Taus serikali imetoa leseni 125,621 zimetolewa kwa wajasiliamali ukiwezesha upatikanaji wa mikopo ya halmashauri yenye thamani ya Sh bilioni 33,454,296,309 kwa vikundi 3,776 vya wanawake vijana na walemavu. TRA na usarimishaji bodaboda Dk Gwajima amesema kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) maofisa usafirishaji waendesha bodaboda na bajaji 209,632 wamerasimishwa kwa kupatiwa leseni za udereva.
Amesema katika kurasimisha na kuwezesha wajasiriamali serikali imeendelea kushirikiana na taasisi za kifedha kutoa mikopo. Dk Gwajima alisema urasimishaji umewezesha wajasiriamali kunufaika na benki za biashara ikiwemo NMB. Amesema wajasiriamali 511,898 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya bilioni 646.7, katika Benki ya Biashara Tanzania (TCB) wajasiriamali 1,418 walipata mikopo ya bilioni 56 na Benki ya DCB wajasiriamali 1,752 walipata bilioni 4.5.
Viwanda na Biashara Dk Gwajima amesema Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) wajasiriamali 16,325 wakiwemo wanawake 8,462 na wanaume 7,863 wamerasimishwa huku wajasiriamali 11,000 kupatiwa mafunzo na ujuzi wa biashara na wajasiriamali 12,325 walipata mikopo kukuza mitaji na wajasiriamali 3,900 walipatiwa namba za mlipakodi (TIN) na leseni za biashara.
Hatua hiyo imeongeza kiwango cha urasimishaji, kuimarisha ajira binafsi na kuweka misingi ya ukuaji wa biashara ndogondogo. “Kuanzia Novemba Mosi, 2025 hadi Januari 23, 2026, SIDO ilitoa mikopo 265 kwa wajasiliamali kupitia Mfuko wa Kuendeleza Wananchi na Mfuko wa Dhamana ya Serikali ya thamani ya Sh bilioni moja na kutoa ajira 652 huku vijana wakinufaika na ajira 489,” alisema.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk Gwajima amesema TBS imewezesha upatikanaji wa mafunzo ya uzalishaji bidhaa kwa ubora na usimamizi wa biashara 1,059 na bidhaa 192 zilipewa nembo ya ubora na kuingia sokoni kwa ajili ya ushindani. SOMA: Gwajima atoa neno kifo cha mtoto Dodoma
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Gwajima alisema katika uvuvi wajasiriamali 4,578 wamerasimishwa wakiwemo wavuvi ni 2,100, wafugaji viumbe maji 2,478, vyama vya ushirika vya mashamba ya mifugo 126 na mashamba ya mifugo 173,147. Alisema vijana 317 wamerasimishwa na kuwezeshwa katika uwekezaji wa miradi ya ufugaji samaki kati ya hao 164 katika vizimba na 153 katika ufugaji wa jongoo bahari, kilimo cha mwani na kunenepesha na serikali imetoa bilioni saba kuwezesha miradi hii ya BBT.
Dk Gwajima amesema kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) vijana 282 wakiwemo wanawake 80 na wanaume 202 wamerasimishwa na kuwezeshwa kufanya kilimo biashara katika shamba lenye ukubwa wa ekari 6,465 lililopo Kaliua mkoani Tabora.
Pia, amesema wakulima 532,023 wakiwemo wanawake 171,705 na wanaume 360,318 wamesajiliwa na kurasimishwa katika mfumo wa ruzuku ya mbolea na kuwezesha kutambua wakulima wanaotumia pembejeo na mbolea inayohitajika. Dk Gwajima amesema katika sekta ya madini wachimbaj wadogo wadogo 2,239 wamesajiliwa na kurasimishwa na kuwezeshwa kupata fursa za mikopo katika taasisi za kifedha ili kukuza mitaji.
PPRA amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imerasimisha vikundi 1,216 vya makundi maalumu katika mfumo wa manunuzi ya umma wa NeST ili washiriki katika zabuni za ununuzi wa umma na kunufaika na asilimia 30 zilizotengwa. Dk Gwajima amesema vikundi 1,123 vilipata zabuni na kwamba vikundi vya wanawake 426 vilipata zabuni za bilioni 13.7, vijana 630 vilipata bilioni 15.4, walemavu 25 milioni 233.2 na wazee 42 bilioni 1.7.
