MAHAKAMA ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam imewapandisha kizimbani watu wawili wakikabiliwa na mashitaka ya kusafirisha bangi aina ya skanka pakiti 20 za uzito wa kilogramu 20.03. Washitakiwa katika shauri hilo namba 1535/2026 la mwaka 2026 ni mkazi wa Buza, Amasha Mrisho (40) na Raia wa Msumbiji Seleman Ally (32).
Wakili wa Serikali, Nicas Kihembe aliwasomea washitakiwa hao mashitaka yao wiki iliyopita mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Lukosi washitakiwa walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza. Akisoma mashitaka hayo wakili Kihembe alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na shitaka moja ambalo ni kusafirisha dawa za kulevya.
Amedai kuwa Desemba 8, 2025 katika operesheni Mtaa wa Wailes, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) waliwakamata washitakiwa wakihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya. Ilidaiwa wakati wa operesheni hiyo, DCEA ilikamata pakiti 20 za bangi aina ya skanka zenye uzito wa jumla wa kilogramu 20.03, ambazo zilikuwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba, kisha kufichwa katika basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours lenye namba za usajili wa Msumbiji AAM 297 CA.

Imedaiwa kuwa zaidi ya vitendo vinavyowakabili washitakiwa ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 16 (I) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inayokataza umiliki, usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya nchini. SOMA: Bibi matatani kilimo cha bangi
Pia, upande wa mashitaka uliieleza mahakama kuwa shitaka hilo halina dhamana kutokana na uzito wa dawa waliokutwa nao washitakiwa, pia uliongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na mashahidi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo siku itakayopangwa. Baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka, mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, washitakiwa walirejeshwa rumande.