CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekithiri katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini. Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Sylivia Daulinge amesema hayo wakati wa mdahalo wa wadau uliofanyika jijini Tanga mwishoni mwa wiki.
Amesema takwimu zinaonesha mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwamo Tanga, Kilimanjaro na Arusha ina kesi nyingi za vitendo vya ukatili kwa kuwa ina asilimia 83 ya kesi za ukatili wa kijinsia. “Takwimu za mwaka 2023 kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga zinaonesha takribani asilimia 33 ya wanawake wamewahi kupitia ukatili wa kijinsia na wa kisaikolojia huku mwenendo ukionesha kuongezeka kwa kasi kwa matukio hayo,” alisema Daulinge. SOMA: Elimu ukatili wa kijinsia yafikia vijana Geita
Amesema Tamwa kupitia mradi wake wa sauti yetu unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ unaangazia kupunguza ama kumaliza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari. Ameongeza kupitia midahalo wanakwenda kujenga uelewa kwa jamii pamoja na wadau wa masuala ya ukatili kuhakikisha wanatoa taarifa za uwepo wa vitendo hivyo, lengo kuu ni kuhakikisha kunakuwa na jamii yenye usalama hususani kwa wanawake na watoto.
Mkuu wa Dawati la Watoto na Jinsia la Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Grace Sandy amesema matukio ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara ni yanayohususu mapenzi katika umri mdogo ambayo ni sawa na ubakaji. “Asilimia kubwa ya kesi za ubakaji zinawahusu wanafunzi ambao ndio wengi hujihusisha na mapenzi katika umri mdogo, jambo ambalo ni kosa kisheria kwa mujibu wa kanuni ya adhabu,” alisema Sandy.
Kaimu Ofisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Lushoto, Beatus Kifumo amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakichangia kuwataka watoto wao wafeli kwa makusudi mitihani, hivyo kukosa haki yao ya kielimu. “Wazazi wanawashawishi wanafunzi wajifelishe na hivyo kushindwa kuendelea masomo kisha wanakwenda kufanya kazi katika umri mdogo, jambo ambalo ni ukatili,” alisema. SOMA:
