WAZIRI wa Afya, Mohammed Mchengerwa amepiga marufuku madaktari wa hospitali za umma kuwaelekeza wagonjwa kununua dawa nje ya hospitali.
Ametolea mfano daktari mmoja wa Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam anayewapeleka wagonjwa kununua dawa nje ya hospitali hiyo.
Mchengerwa amesema serikali haina uhaba wa dawa kwani Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaendelea kusambaza dawa katika hospitali zote nchini, hivyo tabia ya kuwaelekeza wagonjwa kununua dawa nje ni kinyume cha maadili na sheria za kazi.
Aidha, waziri huyo ameagiza hospitali zote nchini kufunga mifumo ya kielektroniki inayosomana ili taarifa za mgonjwa aliyepata matibabu katika kituo kimoja zisomeke katika kituo kingine cha afya.
Hatua hiyo inalenga kuzuia wagonjwa kupimwa vipimo vilevile au kupewa dawa zinazojirudia pasipo sababu za kitabibu.
Mchengerwa alitoa maagizo hayo jana jijini Arusha wakati akikagua Kituo cha Afya cha Kaloleni kwa lengo la kujionea hali halisi ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika ukaguzi huo, alisema kuna daktari mmoja katika Hospitali ya Temeke Dar es Salaam ambaye amekuwa na tabia ya kuwaelekeza wagonjwa kwenda kununua dawa katika duka la dawa lililo jirani na hospitali hiyo, linalodaiwa kumilikiwa na yeye mwenyewe.
“Pale Temeke kuna duka la dawa linalomilikiwa na daktari ambaye anawaelekeza wagonjwa kwenda kununua dawa huko. Nimemwagiza aache mara moja tabia hiyo, asiposikia nitamuondoa yeye kabisa,” alisema Mchengerwa.
Alisisitiza pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma, hospitali zinapaswa kuondoa msongamano wa wagonjwa kwa kuongeza idadi ya watumishi ili wananchi wapate huduma kwa wakati na kurejea kwenye shughuli zao za uzalishaji mali.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa aliagiza Kituo cha Afya cha Kaloleni kiongezwe idadi ya watumishi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa, huku akimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa tano nje ya ukuta wa kituo hicho.
Alisema baada ya ujenzi huo kukamilika, kituo hicho kibadilishwe hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa.
Aidha, alimpongeza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kaloleni, Anna Kimaro kwa kazi nzuri ya utoaji wa huduma za afya, na kumuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe kushirikiana na uongozi wa Jiji la Arusha kukamilisha taratibu za kubadilisha hadhi ya kituo hicho.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla aliwapongeza watumishi wa afya kwa kutoa huduma bora kwa wananchi huku Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk Maduhu Nindwa akisema serikali imetoa Sh bilioni 1.526 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika kituo hicho.
Dk Nindwa alisema ifikapo mwaka 2030, vituo vitatu vya afya mkoani Arusha vitakuwa vinatoa huduma za
afya kwa viwango vya juu, ikiwa ni pamoja na kuzingatia huduma za tiba ya utali.
