Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa ataongeza ushuru wa bidhaa zinazoingizwa kutoka Korea Kusini hadi kufikia asilimia 25.
Hatua hiyo imekuja baada ya kumshutumu Seoul kwa “kutotekeleza ipasavyo” makubaliano ya biashara yaliyofikiwa mwaka jana.
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema ataongeza ushuru huo kutoka asilimia 15 kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo magari, mbao, dawa, na “ushuru mwingine wote wa kulipizana (reciprocal tariffs)”.
Trump alisema kuwa wabunge wa Korea Kusini wamekuwa wakichelewa kuidhinisha makubaliano hayo, ilhali Marekani “imechukua hatua haraka kupunguza ushuru wake kulingana na makubaliano yaliyofikiwa”.
Kwa upande wake, Korea Kusini imesema haijapewa taarifa rasmi kuhusu uamuzi wa kuongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa zake, na imeomba mazungumzo ya haraka na serikali ya Marekani juu ya suala hilo.
Ushuru hulipwa na makampuni yanayoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Katika hali hii, makampuni ya Marekani yatalipa kodi ya asilimia 25 kwa bidhaa wanazonunua kutoka Korea Kusini.
Trump amekuwa akitumia mara kwa mara ushuru kama njia ya kushinikiza au kutekeleza sera zake za kigeni katika muhula wake wa pili Ikulu.
Jumamosi iliyopita, alitishia kuiwekea Canada ushuru wa asilimia 100 endapo ingeingia makubaliano ya biashara na China.
Siku ya Jumatatu, maafisa wa China walisema kuwa makubaliano yao ya “ushirikiano wa kimkakati” na Canada hayalengi kudhoofisha au kuathiri nchi nyingine.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alisema nchi yake haifuatilii makubaliano ya biashara huria na China, na kwamba “haijawahi” kufikiria kufanya hivyo.
Awali, Trump alisema angeweka ushuru wa kuagiza bidhaa kutoka nchi nane, zikiwemo Uingereza, ambazo zilipinga mpango wa Marekani wa kuichukua Greenland, eneo linalojitawala chini ya Ufalme wa Denmark, ambayo ni mwanachama wa NATO.
Baadaye, Trump aliondoa tishio hilo la ushuru kuhusu Greenland, akisema kumekuwa na maendeleo kuelekea “makubaliano ya baadaye” juu ya kisiwa hicho.
Hata hivyo, tukio hilo liliharibu uhusiano wa Marekani na Denmark pamoja na washirika wengine wa NATO.