Diwani wa Kata ya Chanika, Dkt. Habibu Mbota, amekutana na viongozi wa kada ya elimu ya msingi na sekondari katika kata hiyo kwa lengo la kuongoza zoezi la upandaji miti katika shule mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Zoezi hilo lililofanyika katika shule za msingi na sekondari lililenga kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa upandaji miti katika kulinda na kuboresha mazingira, sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kulingana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Dkt. Mbota amesisitiza kuwa kila kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha anaitumikia jamii ipasavyo, akibainisha kuwa masuala ya usafi wa mazingira na utunzaji wa mazingira ndani ya kata ni kipaumbele muhimu.
Aidha, Diwani huyo aliwahimiza wananchi na Taasisi za elimu kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho kinaishi katika mazingira salama na endelevu.
Zoezi hilo lilipokelewa kwa hamasa kubwa na wananchi, walimu pamoja na wanafunzi, huku likiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Dkt. Samia kwa vitendo vinavyogusa moja kwa moja maendeleo ya jamii.

(Feed generated with FetchRSS)