Baada ya karibu wiki mbili hatimaye, Shirikisho la kandanda barani Afrika CAF limetangaza kuchukua hatua kufuatia vurumai lililotokea wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya wenyeji Morocco dhidi ya Senegal mnamo Januari 18. 

CAF imemfungia mechi tano na faini ya dola za kimarekani 100,000 kocha wa Senegal Pape Thiaw   kufuatia  matukio ya vurugu katika mchezo huo wa fainali.

Taarifa ya CAF imesema kwamba kocha huyo ameadhibiwa kwa kufanya mambo kinyume na utaratibu na kuuchafua mchezo ingawa timu yake ya Senegal ilishinda 1-0 baada ya muda wa ziada.

Matangazo ya televisheni ya fainali yalionyesha Thiaw akitoa ishara kwa wachezaji wake wakati Morocco ilipopewa penalti wakati wa dakika za nyongeza baada muda wa kawaida wa dakika 90. Kitendo hiki kimetafsiriwa kwamba ni kama yeye aliitaka timu yake iondoke uwanjani.

Mbali na Kocha Thiaw, washambuliaji wa Senegal Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr, wanaocheza Ligi Kuu ya Uingereza, wamefungiwa mechi mbili kwa “tabia isiyo ya kimichezo dhidi ya mwamuzi”.

Senegal I AFCON I 2025
Kocha wa Senegal Pape ThiawPicha: Misper Apawu/AP Photo/picture alliance

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) nalo limetozwa faini ya jumla ya dola 615,000 kwa makosa mbalimbali wakati wa fainali.

Makosa hayo ni pamoja na tabia zisizo za kimichezo kwa wachezaji wao na wafanyakazi wa benchi la ufundi kinyume na kanuni za nidhamu za CAF za mchezo wa haki, uaminifu na uadilifu.

Morocco nayo yapigwa rungu

Morocco pia haijasalimika katika rungu hili la CAF kwa tabia zisizo ya kimichezo. Mshambuliaji wa Morocco Ismael Saibari alipigwa marufuku ya mechi tatu na faini ya dola 100,000, huku nahodha wa Simba hao wa Atlas Achraf Hakimi akisimamishwa kwa mechi mbili.

Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limepigwa faini ya dola 200,000 kwa tabia zisiyofaa.

Faini ya ziada ya dola 100,000 imewekwa pia kwa wachezaji na wafanyakazi wa benchi la ufundi waliovamia eneo la ukaguzi wa VAR na kumzonga zonga mwamuzi wa Kongo aliyekuwa anatizama picha za marudio.

Senegal I Morocco
Mshambuliaji wa Morocco Brahim Diaz akifoka wakati wa mjadala kuhusu penati kwenye fainali ya AFCONPicha: Sebastien Bozon/AFP/Getty Images

Pia kuna faini ya dola 15,000 baada ya mashabiki wa Morocco kutumia tochi za mwanga mkali kujaribu kuwavuruga wachezaji wa Senegal, na hivyo kufanya jumla ya jumla faini kwa Morocco kufikia dola za kimarekani 315,000.

Fainali ya AFCON kati ya Morocco na Senagal ilichukua sura mpya mwishoni mwa mchezo baada Seenagal kukataliwa goli na muda mchache Morocco kupatiwa penati ambayo ilizusha vurugu. Baadaye Morocco walicheza penati hiyo ambayo ilidakwa na mlinda lango wa Senegal Edou Mendy. Mechi hiyo ilienda kwenye muda wa ziada na Pape Gueye akafunga bao na kuipa Senegal taji la pili la AFCON.

Hata hivyo, adhabu kwa kocha wa Senegal na wachezaji hao wanne yanahusisha tu mechi za CAF na kwamba hazitaathiri maandalizi ya Senegal na Morocco kwa Kombe la Dunia la 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *