
Uturuki iko tayari “kuimarisha usalama kwenye mpaka wake” na Iran iwapo kutatokea shambulio la Marekani, afisa mkuu wa Uturuki ameliambia shirika la AFP leo Alhamisi Januari 29.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nchi hizo mbili zinashiriki zaidi ya kilomita 500 za mpaka, sehemu yake ikiwa imehifadhiwa na ukuta mrefu unaotenganisha nchi hizo mbili kwa takriban kilomita 380, “lakini hii haitoshi,” afisa huyo mkuu amesema kwa sharti la kutotajwa jina.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anatarajiwa siku ya Ijumaa nchini Uturuki, ambayo inatarajia kuchukua jukumu la upatanishi katika kupunguza mvutano kati ya Tehran na Washington, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ametangaza siku ya Alhamisi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan ataonyesha upinzani wa Uturuki kwa uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Iran, akibainisha hatari ambazo mpango kama huo unaleta kwa eneo hilo na dunia, na atasema kwamba Uturuki iko tayari kuchangia katika kutatua mvutano wa sasa kupitia mazungumzo, chanzo hicho kimesema.
Iran itaziona nchi jirani kuwa “adui” ikiwa ardhi zao zitatumika kwa mashambulizi
Iran itazichukulia nchi jirani kama “adui” ikiwa “ardhi zao, anga, au maji vitatumika” kwa mashambulizi dhidi ya nchi hiyo, afisa mkuu katika Jeshi la majini kutoka Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alionya siku ya Jumanne, kulingana na shirika la habari la Iran la FARS.
“Ujumbe huu umewasilishwa” kwa nchi katika eneo hilo, aliongeza Mohammad Akbarzadeh, akitishia kuzuia Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya maji kwa usafiri wa nishati, iwapo kutakuwa na shambulio.