
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, siku ya Jumatano, Januari 28, 2026, amewasihi wapinzani aliowaelezea kama “watu wenye msimamo mkali” “kubaki mjini Washington,” akimrejelea kiongozi wa upinzani na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Maria Corina Machado.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Bi. Rodriguez alitoa maonyo haya wakati wa sherehe iliyohudhuriwa na wanajeshi wapatao 3,200 huko Fuerte Tiuna, kambi ya kijeshi huko Caracas ambapo Rais Nicolás Maduro alikamatwa Januari 3 na jeshi la Marekani. Wakati wa sherehe hiyo, waliapa utii kwake.
“Wale wote wanaoipenda Venezuela kweli waje, lakini wale wanaotaka kuendeleza madhara na uchokozi dhidi ya watu wa Venezuela wabaki Washington!” alitangaza, akishutumu “msimamo mkali.”
“Hawataingia hapa kuharibu amani na utulivu wa Jamhuri: kutakuwa na sheria na kutakuwa na haki,” alitishia.
“Tuko wazi kuelewa, tuko wazi kwa mazungumzo, lakini hatuko wazi kwa uchokozi zaidi,” aliongeza.
Bi. Machado aliunga mkono uingiliaji kati uliosababisha kukamatwa kwa Nicolas Maduro. Operesheni ilioendeshwa na jeshi la Marekani Januari 3. Siku ya Jumatano, alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio huko Washington, baada ya hapo aliwaambia waandishi wa habari, “Nadhani hakuna anayemwamini Delcy Rodríguez.”
Akiwa amepigwa marufuku kugombea katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024, kiongozi huyo wa upinzani alilazimika kujificha kabla ya kuondoka nchini ili kuhudhuria sherehe yake ya Tuzo ya Nobel huko Oslo mnamo mwezi Desemba, na baadaye akawasili Marekani.
Hata hivyo, Washington ina uhusiano usioeleweka na kiongozi huyu mkuu wa upinzani, ikisema inamuunga mkono lakini ikipendelea kushughulika na mamlaka ya mpito hadi itakapochukuliwa hatua nyingine.
Siku ya Jumatano, Bw. Rubio alitetea sera hii, akitaja “maendeleo ya kuridhisha” katika uhusiano wa Marekani na mamlaka huko Caracas.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Januari, Bi. Rodriguez amesaini mikataba ya mafuta na Marekani, akaahidi mageuzi ya kisheria na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, na kufanya uteuzi mwingi.
“Jeshi na polisi waonyesha uaminifu na utii wao kwa rais Rodriguez”
Wakati wa sherehe hiyo siku ya Jumatano huko Caracas, jeshi na polisi kwa mara nyingine waliapa uaminifu wao kwa rais wa mpito. “Tunaapa uaminifu na utii kamili,” alitangaza Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino Lopez, ambaye alimpa Bi. Rodriguez kijiti kinachoashiria amri kuu ya vikosi vya jeshi pamoja na upanga wa Simón Bolívar, shujaa wa uhuru wa Venezuela.
Waziri mwenye nguvu wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello pia alionyesha uaminifu wake kwa Bi. Rodriguez kwa niaba ya polisi, akisema: “Uaminifu wetu kwa Katiba ya taifa na rais wake wa mpito ni kamili, kwa sababu tunaelewa kwamba kutetea matendo yake kunamaanisha kutetea mwendelezo wa serikali na uadilifu wa raia wa Venezuela. (…) Chini ya uongozi wake, tutahakikisha kwa ufanisi utulivu wa ndani na ulinzi wa raia.”
Jeshi tayari lilebainisha kumuunga mkono Bi. Rodriguez mapema Januari 4.
Siku ya Jumatano Bw. Rubio alisema wakati wa kikao mbele ya kamati ya bunge kwamba alifikiria uwepo wa kudumu wa kidiplomasia wa Marekani nchini Venezuela katika “siku za usoni, ambao utaturuhusu kupata taarifa za wakati halisi na kuzungumza na mamlaka ya Venezuela pamoja na wanachama wa mashirika ya kiraia.”
Wiki iliyopita, Marekani ilimteua Laura Dogu, balozi wa zamani wa Nicaragua na Honduras, kama mwakilishi wa Venezuela, ambaye kwa sasa anaishi Bogotá, nchini Colombia.
Nchi hizo mbili hazijawa na uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 2019, kufuatia kuchaguliwa tena kwa Bw. Maduro kwa mara ya kwanza, uchaguzi ambao Washington ilidai uligubikwa na udanganyifu na kusababisha mfululizo wa vikwazo.