Wizara ya Sheria ya Marekani (DOJ) Ijumaa ilitoa idadi kubwa ya nyaraka mpya zinazohusiana na uchunguzi wa mfadhili tajiri marehemu Jeffrey Epstein, hatua inayolenga kuongeza uwazi kuhusu kile ambacho serikali ilijua juu ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana wadogo na mahusiano yake na watu wenye mamlaka na ushawishi mkubwa.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche, alisema zaidi ya kurasa milioni 3 za nyaraka zimeachiliwa, pamoja na zaidi ya video 2,000 na picha 180,000. Faili hizo zimewekwa kwenye tovuti ya wizara hiyo na ni sehemu ya mamilioni ya kurasa zilizokuwa zimezuiliwa katika awamu ya awali ya taarifa zilizotolewa Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, wabunge wa chama cha Democratic, waliokuwa mstari wa mbele kushinikiza kutolewa kwa faili hizo, wanasema kilichotolewa ni karibu nusu tu ya nyaraka zote zilizokusanywa kuhusu kesi ya Epstein.

Kutolewa kwa nyaraka hizi kunatekeleza Sheria ya Uwazi Kuhusu NYaraka za Epstein, iliyopitishwa baada ya miezi ya shinikizo la umma na kisiasa. Sheria hiyo inaitaka serikali kufungua faili zake zote kuhusu Epstein na mshirika wake wa karibu na aliyekuwa mpenzi wake, Ghislaine Maxwell.

Epstein alijiua katika seli ya gereza la New York Agosti 2019, mwezi mmoja baada ya kushtakiwa kwa mashtaka ya shirikisho ya biashara haramu ya kingono. Maxwell, kwa upande wake, alihukumiwa kwa kusaidia mtandao wa unyanyasaji wa kingono wa Epstein.

USA 2025 | Jeffrey Epstein na Donald Trump 1997
Miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa na mafungamano na Epstein ni rais wa sasa wa Marekani Donald Trump (kulia) katika picha hii iliyopitgwa 1997.Picha: Capital Pictures/picture alliance

Hati zenye mahusiano ya kisiasa

Baadhi ya nyaraka zilizotolewa zinaonyesha mawasiliano kati ya Epstein na watu wa karibu wa kisiasa. Katika ujumbe wa mwaka 2018, Epstein alibadilishana ujumbe na mshauri wa zamani wa Rais Donald Trump, Steve Bannon, wakijadili jitihada za Trump kumwondoa Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani (Fed), Jerome Powell.

Katika mazungumzo hayo, Epstein alielezea kukerwa kwake na Powell, huku Bannon akiuliza iwapo Powell au Waziri wa Fedha wakati huo, Steve Mnuchin, wangeweza kuondolewa. Trump baadaye alimtaja Kevin Warsh kama mrithi wa Powell.

Nyaraka nyingine zinahusiana moja kwa moja na kifungo cha Epstein na kifo chake. Barua pepe kati ya wachunguzi zinajadili kifo hicho na hata barua ya mwisho ya Epstein, huku ikielezwa kuwa haionekani kama barua ya kujiua. Maelfu ya kurasa kuhusu kifo hicho tayari zilikuwa zimechapishwa awali.

Pia, baadhi ya hati zinahusu malalamiko ya Ghislaine Maxwell kuhusu mazingira ya kifungo chake.

Marekani, Washington D.C. 2025 | Picha ambayo haijawahi kuchapishwa inamuonyesha Bill Clinton akiwa na Jeffrey Epstein na Ghislaine Maxwell
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton (katikati) pia ni miongoni mwa wanaotajwa zaidi kwenye nyaraka za Epstein.Picha: Epstein Estate/House Oversight/ZUMA/IMAGO

Shinikizo kutoka bungeni

Kamati ya Usimamizi ya Baraza la Wawakilishi imetoa wito maalum (subpoena) kwa Mwanasheria Mkuu Pam Bondi kuwasilisha faili zote bila kufutwa sehemu yoyote, lakini agizo hilo bado halijatekelezwa. Mbunge Robert Garcia, Mdemocrat mkuu katika kamati hiyo, alitaja kutolewa kwa sehemu tu ya nyaraka kuwa “kunakera na kunatia wasiwasi mkubwa.”

Mbunge Ro Khanna, aliyedhamini sheria ya uwazi, alisema DOJ imetambua zaidi ya kurasa milioni 6 zinazoweza kutolewa, lakini imetoa takribani milioni 3.5 tu baada ya uhakiki na uhariri, jambo linalozua maswali kuhusu kilichobaki.

Faili hizo pia zinajumuisha vidokezo visivyothibitishwa vilivyotumwa kwa wachunguzi kwa miaka mingi, baadhi vikihusisha madai ya ajabu dhidi ya watu maarufu. Wachunguzi wa FBI walirekodi madai hayo kwa uangalifu, hata kama yalionekana hayana mantiki.

Kama ilivyokuwa kwa nyaraka zilizotolewa awali, sehemu kubwa ya hati hizi imefutwa, ikiwemo majina ya wahanga, taarifa za kitabibu, picha na video nyeti, pamoja na nyenzo zozote za unyanyasaji wa kingono kwa watoto.

Uingereza, Balmoral 2025 | Picha ya Andrew Mountbatten-Windsor akiwa na Epstein na Maxwell yachapishwa
Andrew Mountbatten-Windsor (aliyekuwa Mwanamfalme Andrew), Jeffrey Epstein na Ghislaine Maxwell karibu na Balmoral, nchini Scotland.Picha: House Oversight Committee/Captital Pictures/picture alliance

Wizara ya sheria yajitetea

Todd Blanche alitetea hatua za wizara hiyo, akisema mawakili wa serikali walilazimika kupitia kurasa zaidi ya milioni 6 ili kuhakikisha taarifa za wahanga hazitolewi hadharani. Alikanusha madai kwamba kuna faili za siri zinazofichwa kwa misingi ya usalama wa taifa au sera za kigeni.

“Hakuna hazina ya nyaraka za siri za Epstein tunazoficha,” alisema Blanche, akiongeza kuwa mchakato wa mapitio na uchapishaji ulikuwa “jitihada isiyo ya kawaida.”

Hakuna ratiba kamili ya lini nyaraka zote zitafunguliwa. Mwanasheria wa serikali ya shirikisho Manhattan, Jay Clayton, alisema baadhi ya hati zimezuiwa kwa muda wakisubiri mwongozo zaidi kutoka mahakama za kiraia na jinai.

Wakati huo huo, waandishi wa habari wa shirika la Associated Press, wanaendelea kuchambua nyaraka hizo kwa makini, wakisisitiza ulinzi wa wahanga na kuepuka kusambaza uvumi au taarifa zisizothibitishwa.

Licha ya hatua hii kubwa ya uwazi, mjadala unaendelea: je, kutolewa kwa faili hizi kutatoa majibu kamili, au maswali zaidi yataibuka kuhusu mojawapo ya kashfa kubwa zaidi za kingono katika historia ya kisasa ya Marekani?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *