Je, Ujerumani inawarejeshaje wahamiaji waliokataliwaJe, Ujerumani inawarejeshaje wahamiaji waliokataliwa

Ujerumani haina taasisi maalum inayolingana na Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE), ingawa hali hiyo ingeweza kubadilika iwapo tawi la Bavaria la chama cha mrengo wa kulia mkali, Alternative for Germany (AfD), lingeweza kutekeleza mpango wake.

Inaonekana wazi kuwa chama hicho cha kupinga uhamiaji kimechochewa moja kwa moja na hatua za ICE chini ya utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Kwa mujibu wa waraka wa ndani wa chama hicho uliyoonekana na gazeti la Kijerumani la taz wiki hii, AfD inapendekeza kuanzishwa kwa mamlaka mpya ndani ya polisi ya jimbo la Bavaria itakayojulikana kama “Asyl-, Fahndungs- und Abschiebegruppe (AFA)”, yaani Kikundi cha Hifadhi, Ufuatiliaji na Urejeshaji.

Hata hivyo, swali la ufanisi wa mamlaka hiyo linabaki wazi. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, serikali ya Ujerumani imepitisha mfululizo wa mageuzi ya kisheria yaliyolenga kurahisisha kuwafukuza wahamiaji ambao, kwa mujibu wa mfumo wa kiserikali, wana “nafasi ndogo za kubaki nchini.”

Picha ya kielelezo | Ujerumani, Hamburg 2025 | Mwonekano wa Kituo cha Dublin kwa waomba hifadhi huko Hamburg-Rahlstedt
Mwonekano wa ndani wa chumba chenye vitanda, makabati na meza katika kituo kinachoitwa Dublin huko Hamburg-Rahlstedt wakati wa ziara ya waandishi wa habari. Katika kituo hicho cha Dublin, waomba hifadhi wa kwanza wanasubiri kurejeshwa katika nchi ya Umoja wa Ulaya inayohusika na kushughulikia kesi zao.Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Juhudi hizo zimeongezwa kasi zaidi hivi karibuni, huku Kansela Friedrich Merz pamoja na mtangulizi wake, Olaf Scholz, wakijaribu kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyozuia uhamisho wa wahamiaji.

Athari zake zinaonekana wazi katika takwimu. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, wahamiaji 21,311 walifukuzwa nchini kati ya Januari na Novemba 2025 — ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. (Kati ya 2023 na 2024, pia kulikuwa na ongezeko la asilimia 22 ya idadi ya waliotimuliwa.)

Zaidi ya hayo, zaidi ya watu 30,000 waliondoka nchini kwa hiari mwaka 2025 baada ya kupewa “Grenzübertrittsbescheinigung”, hati inayowaarifu kuwa wanapaswa kuondoka Ujerumani ifikapo tarehe fulani. Hatua hii huitwa mara nyingi “kujiondoa wenyewe.”

Nani anaweza kufukuzwa nchini?

Kwa ujumla, mhamiaji yeyote asiye na hadhi ya ukaazi halali, au mwomba hifadhi aliyekataliwa ombi lake, anatakiwa kuondoka Ujerumani ndani ya muda uliowekwa (kwa waomba hifadhi, mara nyingi ni mwezi mmoja). Akishindwa kufanya hivyo, anaweza kufukuzwa kwa nguvu.

Ujerumani 2025 | Kufukuzwa kwa pamoja kwenda Pakistan
Familia ikisindikizwa na maafisa wa Polisi wa Shirikisho la Ujerumani (Bundespolizei) kuelekea safari ya ndege ya kufukuzwa kwenda Pakistan. Polisi wa Shirikisho pamoja na wafanyakazi wa Frontex wanasindikiza safari hiyo kwa uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama.Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Hata hivyo, kuna mazingira ya kipekee. Baadhi ya watu hupewa hadhi ya “Duldung” (kuvumiliwa kwa muda), endapo kuna kikwazo cha kisheria au kibinadamu kinachozuia uhamisho wao, kama vile:

  • Kutokujulikana kwa utambulisho wao
  • Uhusiano wa karibu wa kifamilia na mtu mwingine mwenye hadhi ya “Duldung”
  • Sababu za kibinadamu au kiafya
  • Ikiwa tayari wamepata ajira nchini Ujerumani

Takribani watu 180,000 kwa sasa wana hadhi ya “Duldung” nchini Ujerumani.

Uamuzi wa kumfukuza mtu hufanywa na ofisi ya uhamiaji ya eneo husika, ambayo hukagua kama kuna vizuizi vya kisheria. Ikiwa hakuna, tarehe ya kufukuzwa hupangwa — bila kumjulisha mtu anayehusika.

Iwapo mtu huyo amewahi kujaribu kukwepa urejeshaji hapo awali, au mamlaka zinaamini anaweza kutoroka, serikali inaweza kuamuru azuiliwe gerezani hadi siku ya kufukuzwa.

Urejeshaji unatekelezwaje?

Ingawa uamuzi wa kufukuzwa hufanywa na mamlaka za uhamiaji za majimbo, utekelezaji wa uhamisho hufanywa na maafisa wa polisi wa shirikisho.

Katika baadhi ya matukio, ndege maalum hukodiwa kwa ajili ya uhamisho wa pamoja kwenda nchi fulani, huku polisi wakihakikisha watu wa kutosha wanazuiliwa ili kujaza ndege hiyo. Mwaka 2024, takribani wahamiaji 7,300 kati ya 20,100 walifukuzwa kupitia ndege za kukodiwa.

Hatua hii hugharimu serikali fedha nyingi. Kukodi ndege kunaweza kugharimu makumi ya maelfu ya euro, na maafisa kadhaa wa polisi wa shirikisho pia hulazimika kusafiri kuwasindikiza wahamiaji hao.

Katika visa vingi, wahamiaji wanaotazamiwa kufukuzwa hupewa wito wafike ofisi za uhamiaji, ambako afisa wa polisi huwajulisha rasmi kuwa wanahamishwa. Baadaye husindikizwa nyumbani kuchukua nguo na mali zao kabla ya kupelekwa moja kwa moja uwanja wa ndege.

Hata hivyo, katika baadhi ya matukio, polisi hujitokeza nyumbani kwa wahamiaji mapema alfajiri na kuwakamata. Tofauti na ICE nchini Marekani, polisi wa Ujerumani hawavai barakoa na huvaa sare rasmi. Pia wanatakiwa kubeba vitambulisho vyao na kutoa majina yao wakitaka.

Ujerumani 2025 | Kufukuzwa kwa pamoja kwenda Pakistan kwa usindikizaji wa Polisi wa Shirikisho na Frontex
Wakati mwingine serikali inalaazimika kukodi ndege nzima kuwasafirisha wahamiaji wanapokuwa wengi kutoka nchi moja.Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Kuna simulizi nyingi zinazoonyesha jinsi hali hii ilivyo ya kuumiza kisaikolojia. Msimamizi mmoja wa zamani wa makazi ya wahamiaji aliieleza DW, kwa sharti la kutotajwa jina, tukio ambapo polisi walifika saa 11 alfajiri na kumchukua mwanaume mlemavu moja kwa moja hadi uwanja wa ndege, wakimuacha mke wake — ambaye pia ni mlemavu — bila mlezi wake mkuu.

Kisheria, mtu anayefukuzwa anaruhusiwa kupiga simu kabla ya kuondoka, na katika baadhi ya matukio, mawakili wamefanikiwa kuingilia kati dakika za mwisho kuzuia uhamisho. Hata hivyo, pia kumekuwa na taarifa za watu kunyang’anywa simu zao.

Je, urejeshaji umeharakishwaje?

Katika miaka 10 iliyopita, serikali ya Ujerumani imechukua hatua kadhaa kuharakisha uhamisho wa wahamiaji:

2015: Sheria ilibadilishwa kupanua sababu za kumweka mtu kizuizini kabla ya kufukuzwa.

2016: Msamaha wa kiafya ulipunguzwa, na sasa ni wagonjwa wa kudumu au walioko katika hatari ya maisha pekee wanaolindwa.

2019: Sheria iliruhusu kuzuiliwa mapema kwa wale wanaochukuliwa kuwa wanaweza kutoroka, na pia ikafanya kuwa kosa la jinai kutoa taarifa kuhusu uhamisho uliopangwa.

2022: Waomba hifadhi wanaochukuliwa kuwa hatari waliruhusiwa kuzuiliwa mapema hadi miezi sita.

2024: Polisi walipewa mamlaka ya kupekua vyumba vingine katika makazi wakimtafuta mtu wa kufukuzwa.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hata hivyo, mtafiti Svenja Schurade kutoka Chuo Kikuu cha Göttingen alisema hatua hizo si kwamba zimeharakisha uhamisho katika matukio yote.

“Utafiti wetu unaonyesha kuwa hatua hizi hazijafanya uhamisho kuwa wa ufanisi zaidi,” alisema.

“Badala yake, zimesababisha kutengwa zaidi kijamii na kuwaweka watu katika hali ngumu zaidi za maisha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *