Muhoozi aishtumu Marekani kumficha Bobi Wine, aomba radhiMuhoozi aishtumu Marekani kumficha Bobi Wine, aomba radhi

Mkuu wa Jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba, amejikuta katikati ya mjadala mkali baada ya kuomba radhi hadharani kwa Marekani kufuatia ujumbe aliouchapisha na baadaye kuufuta kwenye mtandao wa X.

Katika ujumbe huo wa awali, Kainerugaba aliutuhumu ubalozi wa Marekani nchini Uganda kwa kusaidia kumficha kiongozi wa upinzani Bobi Wine.

Katika kauli yake ya kuomba radhi, Kainerugaba alisema alipotoshwa na taarifa zisizo sahihi. Aliongeza kuwa amezungumza moja kwa moja na balozi wa Marekani nchini humo na kusisitiza kuwa mahusiano kati ya jeshi la Uganda na Marekani yako salama. Kauli hiyo ilikuja saa chache tu baada ya kutangaza kusitisha ushirikiano wote na ubalozi huo.

Kabla ya kubadilisha msimamo, Kainerugaba alikuwa ameandika kwamba jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Uganda (UPDF) lingesimamisha ushirikiano wote na Marekani, ikiwemo operesheni za pamoja nchini Somalia ambako Uganda ina mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya waasi wa kundi la Al-Shabaab.

Kauli hizi zilichochewa na madai kwamba Bobi Wine, kiongozi wa upinzani, alikuwa “amejiteka mwenyewe” kwa ushirikiano na Marekani. Taarifa hizo zilikanushwa vikali na upinzani na mashirika ya haki za binadamu.

Mvutano huu unajiri katika mazingira ya uchaguzi wa rais uliofanyika Januari 15, ambao upinzani umedai ulikumbwa na wizi wa kura, kuzimwa kwa huduma za intaneti na matumizi makubwa ya jeshi kwenye mchakato wa uchaguzi.

Entebbe, Uganda 2024 | Maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Jenerali Muhoozi Kainerugaba
Rais Yoweri Museveni akitazama huku Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mke wake Charlotte na mama yake Janet Museveni wakikata keki ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa katika Ikulu ya Entebbe.Picha: Ugandan Presidential Press Unit

Uchaguzi tata na kutoweka kwa Bobi Wine

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, aliingia mafichoni muda mfupi baada ya uchaguzi huo. Alidai kuwa wanajeshi walivamia nyumba yake kwa lengo la kumkamata, jambo lililomlazimu kukimbia kwa hofu ya usalama wake.

Katika video alizotoa akiwa mafichoni, Wine alionekana akitembea kwenye makaburi ya familia yake, akimdhihaki mkuu wa jeshi kwa kushindwa kumkamata. Alisema hali hiyo inaonesha udhaifu wa serikali licha ya kuonekana kuwa na nguvu kubwa ya kijeshi.

Wine amepinga matokeo rasmi ya uchaguzi yaliyomtangaza Rais Yoweri Museveni mshindi kwa zaidi ya asilimia 71 ya kura. Museveni, mwenye umri wa miaka 81, sasa anaelekea kuhudumu muhula wa saba, hatua itakayomfikisha karibu miaka 50 madarakani.

Kiongozi huyo wa upinzani amewahimiza wafuasi wake kutumia njia za kisheria kuonesha kutoridhika kwao, akisisitiza kuwa mapambano yao si ya vurugu bali ya kudai haki na uwajibikaji.

Kwa upande wake, Kainerugaba amejibu video na kauli za Wine kwa lugha kali, akimtaja kwa majina ya kudhalilisha na kumwita gaidi. Tabia ya Kainerugaba ya kuchapisha ujumbe wa uchochezi na baadaye kuufuta imekuwa ikijadiliwa sana ndani na nje ya Uganda.

Uganda Kampala | Kutunukiwa Muhoozi Kainerugaba kuwa Luteni Jenerali
Mnamo Februari 19, 2019, Muhoozi Kainerugaba alivishwa nyota ya Luteni Jenerali wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Uganda, UPDF.Picha: Joseph Kiggundu/Photoshot/picture alliance

Hofu ya machafuko na madai ya unyanyasaji

Mvutano kati ya jeshi na upinzani umeongeza hofu miongoni mwa wananchi kwamba shambulio lolote dhidi ya Bobi Wine linaweza kusababisha machafuko makubwa. Wine ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wa mijini wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira na kuchoshwa na utawala wa miongo kadhaa wa kiongozi mmoja.

Hali ilizidi kuwa tete baada ya uvamizi wa Januari 23 nyumbani kwa familia ya Wine, ambapo mke wake, Barbara Kyagulanyi, alidai kupigwa na wanajeshi. Alisema alivutwa, akapigwa na hata kichwa chake kugongwa kwenye nguzo, jambo lililomfanya alazwe hospitalini.

Kainerugaba alikiri kuwa operesheni hiyo ilifanywa na wanajeshi wake lakini alikanusha madai ya kumpiga Barbara. Alisema jeshi halipigi wanawake na kusisitiza kuwa walikuwa wakimtafuta Wine, si mke wake.

Mashirika ya haki za binadamu yameendelea kuishutumu serikali ya Uganda kwa kutumia jeshi kukandamiza upinzani, madai ambayo serikali imekuwa ikiyakataa mara kwa mara.

Jeshi la Uganda linavyojihusisha kwa karibu na uchaguzi mkuu

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mustakabali wa siasa za Uganda

Licha ya shutuma na mvutano, Museveni ameapa kudumisha amani na utulivu nchini humo, akisema upinzani unajaribu kuchochea vurugu. Wafuasi wake wanamsifu kwa kudumisha usalama ambao umeifanya Uganda kuwa kimbilio la wakimbizi wengi kutoka nchi jirani.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa kauli za hovyo kutoka kwa viongozi wa kijeshi, pamoja na matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzani, zinaweza kuathiri taswira ya Uganda kimataifa na kuharibu mahusiano yake na washirika wa muda mrefu kama Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *