
Wapalestina wasiopungua 31, wakiwemo kwa uchache watoto sita, wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel tangu alfajiri ya leo hadi wakati huu katika Jiji la Ghaza na mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Ghaza.
Mashambulio hayo ya leo yamefanyika siku moja kabla ya utawala ghasibu wa Israel kufungua tena kivuko cha Rafah, kinachounganisha Ghaza na Misri kesho Jumapili kwa mara ya kwanza tangu Mei 2024.
Mohammed al-Helou, mkazi wa Jiji la Ghaza, amesema jeshi la kizayuni halikutoa onyo lolote kabla ya kuripua nyumba ambayo ni makazi ya raia usiku wa kuamkia leo.
“Ndege zisizo na rubani za upelelezi na ndege za kivita zilikuwa katika eneo hilo na zikiruka kwenye masafa ya chini sana. Saa kumi alfajiri nyumba hii ya makazi ilipigwa huku familia na watoto wakiwa wangali wamo ndani,” ameeleza al-Halou na kuongezea kwa kusema: “hakuna onyo lolote lililotolewa. Hakuna kitu ambacho watoto wamefanya kustahili kuuawa.”
Mahmoud Basal, ambaye ni msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Palestina huko Ghaza, ameiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba wengi wa waliouawa katika mashambulizi ya Israeli leo ni watoto.
Amesema vikosi vya jeshi la utawala wa kizayuni vilitumia makombora, ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa na moto mkubwa katika maeneo yaliyolengwa.
Basal ameongeza kuwa watu saba hadi sasa wamepatikana kutoka makao makuu ya polisi yaliyoripuliwa na jeshi la Israel katika kitongoji cha Sheikh Radwan cha Jiji la Ghaza.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Ghaza imesema zaidi ya Wapalestina 500 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa kizayuni tangu usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani huko Ghaza ulipoanza kutekelezwa Oktoba 10.
Vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel Oktoba 2023 dhidi ya Ghaza vimewaua watu wasiopungua 71,769 na kuwajeruhi 171,483…/