Jopo la wataalamu wa serikali ya Japani linatoa wito wa idadi ya maeneo yenye hatua dhidi ya utalii wa kupita kiasi kuongezeka maradufu.
Serikali inapanga kurekebisha Mpango wake wa Msingi wa Kukuza Utalii wa Taifa. Jopo hilo la wataalamu liliwasilisha rasimu ya marekebisho hayo katika mkutano wake Januari 30. Hatua hiyo inakuja wakati utalii wa kupita kiasi ukiwa tatizo katika sehemu nyingi za nchi hiyo, huku idadi ya watalii wa kigeni ikiendelea kuongezeka.
Rasimu hiyo inasema changamoto kuu ni kupata uwiano kati ya kuwakaribisha watalii wa kigeni na kudumisha ubora wa maisha ya wakazi.
Rasimu hiyo inaweka lengo la kuongeza idadi ya maeneo yenye hatua za utalii kupita kiasi kutoka 47 ya sasa hadi 100 ifikapo mwaka 2030. Hatua hizi zinalenga kupunguza msongamano mkubwa na kuwafahamisha watalii kuhusu nidhamu sahihi, miongoni mwa madhumuni mengine.
Serikali pia inapanga kuongeza mara tatu kodi ya kuondoka hadi yeni 3,000, au takribani dola 20. Mapato hayo yanatarajiwa kutumika kufadhili hatua hizo.
Rasimu hiyo inadumisha lengo la serikali la mwaka 2030 la watalii wa kigeni milioni 60, kutoka milioni 42 mwaka jana. Pia inadumisha lengo la matumizi la yeni trilioni 15, au takribani dola bilioni 97.
Serikali inapanga kukamilisha mpango wa msingi ifikapo mwisho wa mwezi Machi baada ya kukusanya maoni ya umma.