Kocha wa timu yya soka ya Manchester City Mhispania Pep Guardiola kwa mara nyingine ametangaza himaya na uungaji mkono wake kwa Palestina na kusisitiza kwamba, yeye yuko pamoja na Wapalestina.

Guardialo amesema hayo katika hafla ya wanaharakati wanaounga mkono Palestina katika pwani ya Barcelona nchini Uhispania na kubainisha kwamba: Ninasema haya wazi kwa kila mtu; Mimi sio kwamba, siko upande wowote, la hasha, bali niko upande wa Wapalestina, ninasimama pamoja na Palestina. Ninasimama pamoja na wanyonge na wanaokandamizwa, na wanaokandamizwa leo ni Palestina.

Katika tukio hilo, meneja wa Manchester City Pep Guardiola, ambaye alikuwa akihudhuria kampeni ya hisani huko Barcelona, alitoa hotuba athirifu kuhusu uhalifu wa utawala wa Israeli huko Gaza na kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kibinadamu na waathiriwa wa vita.

“Ninapomwona mtoto katika kipindi cha miaka miwili iliyopita akiuliza kupitia picha na vyombo vya habari kuhusu mama yake aliyezikwa chini ya kifusi, nahisi kwamba tumewaacha peke yao; wameachwa na kupuuzwa. Mtoto anauliza: Uko wapi? Njoo utusaidie. Na hadi sasa hatujafanya hivyo,” Guardiola alisema.

Akihutubia huku akiwa amevaa skafu ya Keffiyeh ambayo ni nembo ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina wanaoendelea kuuawa na majeshi ya Israel, kocha huyo wa klabu ya Manchester City ya Uingereza alisisitiza haja ya kushiriki na kusimama na wanyonge zaidi, akisema: “Suala hili si la Palestina tu, bali linajumuisha masuala yote ya kibinadamu.”

Meneja wa Manchester City alisisitiza kwamba lengo la mabomu na ukimya wa kimataifa ni kupuuza ukweli.

“Labda ni kwa sababu walio madarakani ni waoga na huwatuma vijana wasio na hatia kuwaua wengine huku wao wenyewe wakifurahia joto au kiyoyozi majumbani mwao. Tunahitaji kupiga hatua mbele, na uwepo wetu pekee una thamani kubwa,” aliongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *