
Nchini Mali, msafara mpya wa malori yanayosafirisha mafuta ulilengwa katika shambulio lililohusishwa na wapiganaji wa jihadi kutoka Kundi linalodai kutetea Uislamu na Waislamu (JNIM), mshirika wa Al-Qaeda. Shambulio hilo lililotokea katika eneo la Kayes magharibi mwa Mali, kwenye barabara inayoelekea mpaka wa Senegal, lilisababisha vifo kadhaa.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nchini Mali, wapiganaji wa kijihadi kutoka Kundi linalodai kutetea Uislamu na Waislamu (JNIM), mshirika wa Al-Qaeda, wanaanza tena mashambulizi yao dhidi ya misafara ya malori yanayosafirisha mafuta. Siku ya Alhamisi, Januari 29, malori mengi ya mafuta yaliharibiwa katika eneo la Kayes magharibi mwa Mali.
Shambulio hilo pia lilisababisha waathiriwa kadhaa: huku afisa wa eneo hilo akinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kwamba wanajeshi watatu wa Mali na washambuliaji wanne waliuawa, miili miwili ya raia pia ilipatikana siku ya Ijumaa kwenye barabara inayounganisha Kayes na mpaka wa Senegal. Wanajeshi kadhaa waliokuwa wakisindikiza msafara huo bado hawajulikani walipo, anaripoti mwandishi wetu wa kikanda Serge Daniel.
Ingawa afisa kutoka Ofisi ya Bidhaa za Petroli nchini Mali, pia alinukuliwa na shirika la habari la AFP, alidai kwamba shambulio hilo “haliiathiri usambazaji au upatikanaji” wa mafuta, shambulio hili hata hivyo linaonesha pigo lingine kwa serikali. Shambulio hilo ambalo lilitokea chini ya wiki tatu kabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, pia linakuja siku 10 tu baada ya mamlaka kutangaza utekelezaji ujao wa mfumo wa mgao wa mafuta. Hatua hiyo inajumuisha hasa kupunguza idadi ya ziara zinazoruhusiwa kwenye vituo vya mafuta kuwa kila baada ya siku tatu kwa magari na kila baada ya siku mbili kwa pikipiki. Lengo? “Kupunguza ununuzi mwingi na kupambana na njia za mauzo haramu,” kulingana na Serikali ya Mpito.
Kayes, eneo la kimkakati
Kwa zaidi ya miezi minne, wanajihadi wa JNIM wameweka kizuizi cha kiuchumi kusini na magharibi mwa Mali, maeneo mawili ambayo usafirishaji wa mafuta kutoka Senegal na Côte d’Ivoire hupitia.
Lakini tangu mwanzoni mwa mwezi Januari, mashambulizi ya jihadi yameongezeka tena, na kuinyima mji mkuu wa Mali na miji mingine nchini mafuta. Matukio haya yalitokea katika eneo la Kayes, eneo la kimkakati kutokana na rasilimali zake za madini na nafasi yake kama njia panda.