Dar es Salaam. “He who finds a wife finds a good thing” ni maneno yenye maana ya ‘Yeye apataye mke hupata kitu chema’. 

Mara nyingi furaha hiyo kwa wawili wanaopendana haiishii kwao tu. Bali hufika hadi kwa wazazi wao. Hilo limejionesha Edward Mwakionde baba wa mwanamuziki Miriam Chirwa ambaye hivi karibuni ametangaza kuchumbiwa na kujikuta akiingia kwenye dhihaka za watu kutokana na mwonekano wake.

Akizungumza na Mwananchi baba wa msanii huyo wa nyimbo za injili aliyewahi kutamba na vibao kama Unitambulishe Yesu, Elimu ni Mwanga, Nina Wimbo na nyinginezo amesema amefurahi binti yake kutimiza ndoto ya kupata mwenza.

“Hili jambo la kuchumbiwa Miriam amelileta kama mara nne kwangu. Wapo vijana ambao walimdhihaki na kumsononesha moyo, alipowaambia kama wapo tayari kumuoa basi walete barua wakaenda kushoto.

“Wakaenda kumdhihaki sana, wakamwambia anadhani yeye ni mwanamke ambaye wanaweza kuongozana nao? Wengine wakasema walitaka kumpima tu ili aingia mkenge. Kama familia tukanyamaza. Lakini ilipotokea hili la sasa na kijana amejitoa mimi nikafurahi kwamba ndoto ya mwanangu kumpata mwenza wake imetimia,”amesema.

Amesema anampenda binti yake hivyo anampenda na anayemuoa haijalishi ana hali hali gani.

“Hao vijana niliokwambia wote wanne wapo vizuri, hawana tofauti yoyote ya mwili wao. Lakini walimdhihaki binti yangu. Hawakufika nyumbani walikuwa wanaishia njiani wanaonekana walikuwa na utoto sana wakati mwenzao ni mkubwa,”amesema baba huyo.

Hata hivyo, tangu zisambae taarifa za Miriam kuolewa zimeibuka komenti za dhihaka na kejeli kwenye mitandao ya kijamii. Jambo lililofanya msanii huyo kushindwa kuvumilia hadi familia yake kumtaka kukaa mbali na simu kwa kipindi hiki hadi atapokuwa sawa.

Hili pia lilijidhihirisha Januari 28, 2026 baada ya Mwananchi kumtafuta baba yake kwa ajili ya kuzungumza na binti yake ndipo majibu yalikuwa.

“Upepo umekuwa mkubwa mambo yamekuwa mengi, dhihaka pia zimekuwa nyingi hata alivyozisoma komenti zimemkosesha amani kuna watu wameongea vibaya. Nilichokifanya nimemkataza kusoma komenti kwa sababu kuna jambo lake analisubiri tunaweza tukafelishana. Dhihaka zinavyoendelea zinaweza zikamletea shida ngoja tuone itakavyokuwa kesho,”alisema baba Mariam

Miriam akiwa na mume wake mtarajiwa

Hata hivyo baada ya kutafutwa tena siku iliyofuta kwa ajili ya kuongea na Miriam ilishindikana na ndipo baba huyo alizungumza kwa ajili ya kulinda afya ya akili ya mwanaye

“Miriam anachangamoto ya macho lakini pia alizaliwa njiti. Akaumwa hapo kati Mungu akaruhusu awe na mwili wa bajeti ndogo mimi huwa nauita hivyo kwa sababu hautumii vitu vingi hata kama ni kitambaa. Sasa changamoto ambazo mtu anazipata ni mafuta, ngazi  na ni hodi ya kufungua mlango mwingine ukizitazama kwa jicho chanya.

“Lakini ukizitazama kwa jicho hasi utatengeneza uadui na watu kumbe wao wametumika ili uendelee kun’gara. Wito wangu ni kwamba watu wasije wakarudishwa nyuma kwa sababu ya maneno ya watu. Tupokee kwa chanya ukiangalia vizuri yanaweza kukuvumbulia jambo ili upenye kwenye jambo jingine,”amesema baba Miriam

Amesema kwa ambayo yanaendelea sasa mitandaoni dhidi ya mwanaye ni ngumu kuyazuia kwani wengine wanaongea kujifurahisha.

“Ukiwazuia kusema hutaona upande wa pili wa bahari. Hakuna sababu ya kuanza kusononeka na nguvu zipotee watu watumie akili sana. Miriam ni  wa kawaida watu wameongea fikiria kama viongozi wa dini wanasemwa wa serikali, Yesu Kristo na hata Mohamad walidhihakiwa kwa hiyo Miriam ni nani asisemwe. Hauwezi kumzuia mtu kusema kilichopo moyoni mwake,”amesema. 

Ishu ya mahari
Lipo swali wanalojiuliza watu wengi kuhusu kiasi cha mahari alicholipiwa msanii huyo hapa baba yake anajibu.

“Mahari ni siri ya familia mtoto hauzi. Sio kwa sababu ana jina sana nichukue mahari kubwa. Huyu kijana mimi ni mtoto wangu pia anapokea majukumu ambayo Miriam alikuwa akihudumiwa. Mimi nitatoa huduma pale ambapo inabidi nifanye. Tena nikikwambia mahari utacheka lakini sisemi maana mahari sio kitu cha kupeleka kadamnasi.

“Masuala ya kuanza kukagua mkwe kila mmoja ana ustaarabu wake. Binti yangu aliniambia wamependana nikamuuliza kwa makini. Akanihakikishia ameridhika na huyo bwana na maisha yalivyo mimi kijana wa watu sitaki kumuuliza maswali ambayo anatakiwa kuulizwa huko na mwenzake,”amesema.

Akizungumzia kuhusu tarehe ya harusi ya binti yake huyo ambaye amezaliwa mwaka 1998. Baba Miriam amesema itafanyika Mei 17,2026, huku akieleza taarifa za  kanisa gani ndoa hiyo itafungiwa wataliweka wazi baada ya mambo kukaa sawa.

“Miriam hapendi dharau kama baba yake, uvumi na uzushi hapendi kuvaa nguo za kuonesha maungo ni maadili ambayo hayapendi. Kuhusu safari yake ya muziki kuna wimbo unakuja wiki ijayo ambao ni video na audio ukijibu maswali ya watu kulingana na vigezo vyake vile 15 alivyosema.

“Atawaambia pia kwanini alitoa vile vigezo na watu watajua kama mchumba wake kakidhi vigezo vyake 15. Na baada ya watu kudhihaki wimbo ‘Naenda’ ule wimbo sasa umetengenezwa kuwa kamili na utakuwa tayari baada ya siku nne,”amesema.

Picha ya pamoja Miriam akiwa na baba yake kulia, kushoto mumewe mtarajiwa

Utakumbuka Miriam amewahi kueleza kuwa mwanaume atayeruhusu amuoe ni yule atakayetimiza vigezo 15.  

“Mcha Mungu, nataka mwanaume ambaye akili yake inafanya kazi sawasawa haiishi kitandani unajua kuna mwingine akiamka asubuhi akili yake anaiacha kitandani anakuwa akaamka yeye. 

“Nataka mtu ambaye ni mrefu maana mimi mfupi, atayekubali hivi nilivyo, sitaki mtu aniambie sitaki ufanye hivi, awe baba bora, asiwe mvivu, ajue namna ya kutafuta pesa, awe anapenda watoto,”Miriam alieleza baadhi ya vigezo vyake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *