
Dar es Salaam. Mtetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania, Onesmo Olengurumwa, ametajwa kuwa miongoni mwa wagombea wanaopewa nafasi kubwa kushika wadhifa wa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa (UN) anayeshughulikia hali ya watetezi wa haki za binadamu duniani.
Olengurumwa ameshika nafasi ya pili katika orodha ya waliopendekezwa na Kundi la Ushauri la UN kwa Rais wa Baraza la Haki za Binadamu, kufuatia mchakato wa ushindani uliowahusisha wataalamu 65 kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumzia hatua hiyo, Olengurumwa amesema ameipokea kwa mtazamo chanya, akieleza kuwa ni hatua muhimu kwa kazi ya utetezi wa haki za binadamu Tanzania kufika katika jukwaa la kimataifa.
“Nimeipokea kwa mtazamo mzuri na nina matumaini mchakato utaenda vizuri. Hatufanyi kazi hii kwa ajili ya nafasi au manufaa binafsi, bali kuendeleza huduma tulizokuwa tukitoa kitaifa hadi ngazi ya kimataifa,” esema.
Ameongeza kuwa uteuzi huo unatoa fursa ya kupata uzoefu mpya na kuchangia mageuzi katika ajenda ya haki za binadamu duniani.
Nafasi hiyo ya UN inahusisha kufuatilia ukiukwaji wa haki za watetezi wa haki za binadamu, kushirikiana na serikali mbalimbali pamoja na kuimarisha viwango vya kimataifa vya ulinzi wa nafasi ya kiraia.
Olengurumwa amesema kufikia hatua ya mwisho baada ya mchakato wa usaili na tathmini mbalimbali ni mafanikio makubwa kwa watetezi wa haki za binadamu nchini.
“Hatua yenyewe ya kufika hapa, baada ya mchakato mgumu lakini ulio wazi, ni hatua muhimu. Ninalichukulia kama ni utambuzi wa kazi ya watetezi wa haki za binadamu Tanzania,” amesema.
Olengurumwa ni mwanzilishi na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), pamoja na Katibu wa Bodi ya mtandao huo. THRDC ilianzishwa mwaka 2012 ikiwa na wanachama 14 na kufikia mwaka 2025 imekua na mtandao wa takribani mashirika 300 nchi nzima.
Mtandao huo unajumuisha watetezi wa ngazi ya jamii, waandishi wa habari, makundi ya wafugaji na jamii zilizotengwa, na umejipatia kutambuliwa kitaifa na kimataifa kwa kazi za utetezi wa sera na ulinzi wa watetezi walioko hatarini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, THRDC imewafikia zaidi ya watetezi 10,000 ndani ya kipindi cha miaka 12, huku maelfu wakipata mafunzo ya uelewa wa sheria, usalama binafsi na usalama wa kidijitali.
Kitaaluma, Olengurumwa ni mwanasheria aliyehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ana uzoefu wa utafiti na sera za umma. Aliwahi kufanya kazi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 kabla ya kushiriki kuanzisha THRDC.
Amewahi kushiriki katika mashauri ya kimkakati na mijadala ya sera kuhusu upatikanaji wa haki, uhuru wa kujieleza, haki za watoto, watu wenye ulemavu, haki za wafugaji na jamii zilizotengwa, pamoja na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya hivi karibuni ni uamuzi wa Mahakama ya Rufani wa Juni 2025 ulioondoa baadhi ya vifungu vilivyokuwa vinaweka masharti magumu katika mashauri ya maslahi ya umma, hatua iliyotafsiriwa kuimarisha upatikanaji wa haki za kikatiba.
Mbali na kazi zake ndani ya nchi, Olengurumwa ameshirikiana pia na mifumo ya kikanda na kimataifa ikiwamo Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Baraza la Haki za Binadamu la UN.
Pamoja na mafanikio hayo, amesema kazi ya utetezi imekuwa ikiambatana na changamoto, zikiwamo vitisho, vikwazo na matukio ya kukamatwa, hali inayoonesha umuhimu wa mshikamano wa watetezi wa haki za binadamu duniani.
Wakati uteuzi wa mwisho ukisubiri uamuzi wa Rais wa Baraza la Haki za Binadamu la UN, hatua ya kufika hapa tayari imeandikwa kama historia kwa wanaharakati wa haki za binadamu Tanzania katika jukwaa la kimataifa.