Kiongozi wa mpito wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani, ameituhumu Ufaransa pamoja na nchi jirani za Benin na Ivory Coast kwa kufadhili shambulio la kigaidi lililolenga uwanja mkuu wa kimataifa wa ndege katika mji mkuu wa taifa hilo la Sahel mapema Alhamisi.

Milio ya risasi na milipuko iliripotiwa karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani karibu sita usiku, kabla ya maafisa kutangaza kuwa hali ilikuwa imedhibitiwa.

Baadhi ya ndege zinaripotiwa kuharibiwa, lakini hakuna majeraha makubwa kwa raia yaliyothibitishwa. Televisheni ya taifa ya Niger ilisema kuwa raia mmoja wa Ufaransa alikuwa miongoni mwa washukiwa waliouawa katika makabiliano hayo.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa baada ya kutembelea Kambi ya Anga 101, iliyo jirani na uwanja wa ndege mjini Niamey, Jenerali Tchiani aliwataja Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Patrice Talon wa Benin, na Alassane Ouattara wa Ivory Coast kuwa ndio wafadhili wa shambulio hilo, na akaapa kulipiza kisasi. Kiongozi huyo wa kijeshi alisema, “Tunawakumbusha wale wanaowafadhili mamluki hawa, hususan Emmanuel Macron, Patrice Talon na Alassane Ouattara , kwamba tumewasikia wakibweka kwa muda mrefu vya kutosha; sasa nao wajiandae, kwa upande wao, kusikia tunaponguruma.”

Taarifa zinasema katika ghala la uwanja huo wa ndege kuna tani 1,000 za oksidi ya urani iliyokolezwa, iliyochukuliwa kutoka mgodi wa Arlit na kampuni ya Kifaransa, Orano. Kuna mzozo kuhusu umiliki wa urani hiyo kati ya kampuni ya Kifaransa na serikali ya Niger.

Jenerali Tchiani amesifu vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger, pamoja na wanajeshi wa Russia walioko katika kambi ya kijeshi karibu uwanja huo, kwa “kujibu haraka” na  kuzuia shambulio hilo. Vikosi vya Russia vimekuwa vikihudumu katika kambi hiyo tangu mwaka 2024, baada ya Niamey kusitisha makubaliano ya ulinzi yaliyodumu kwa takriban muongo mmoja na Marekani na kuitaka Washington kuondoa takribani wanajeshi 1,000 wa Kimarekani.

Ufaransa, ambayo hapo awali ilikuwa na satwa ya kibeberu katika eneo la Sahel, imeendelea kupoteza ushawishi wake kutokana na hali ya kutoridhika kwa wananchi kuhusu ukosefu wa usalama, kudorora kwa uchumi, na dhana za kuingiliwa kwa mambo ya ndani na mataifa ya kigeni.

Viongozi wa kijeshi wa Niger, pamoja na washirika wao wa Mali na Burkina Faso, wamewalazimisha wanajeshi wa Ufaransa kuondoka katika maeneo yao, ambako walikuwa wametumwa kupambana na makundi ya kigaidi yanayohusishwa na Al-Qaeda na ISIS.

Nchi hizo tatu zimeunda Muungano wa Mataifa ya Sahel na zimekuwa zikiilaumu Paris mara kwa kulenga kudhoofisha serikali zao kupitia ushirikiano na makundi ya waasi na magaidi katika maeneo ya mipakani. Hadi sasa, Ufaransa, Benin na Ivory Coast bado hazijatoa majibu ya wazi kuhusu tuhuma mpya zilizotolewa na Tchiani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *