
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kwamba, hali ya kibinadamu huko Gaza bado ni mbaya, huku zaidi ya watu milioni moja wakihitaji makazi na msaada wa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti ya OCHA mahitaji ya dharura yanajumuisha zana na vifaa vya kukarabati nyumba zilizoharibika, kuunda nafasi za kijamii za kupasha joto, na vifaa vya kuondoa uchafu ili kuhakikisha hali salama ya maisha kwa wakazi walioathiriwa.
Wiki iliyopita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Umoja wa Mataifa na wadau wa masuala ya kibinadamu waliweza kufikia zaidi ya familia 7,500 na kusambaza mahema, mashuka ya plastiki, vifaa vya kutia joto, magodoro na blanketi. Pia ilitoa nguo za joto kwa takriban watoto 1,400 katika sehemu mbalimbali za Gaza.
Ofisi hiyo iliongeza kuwa mkate hutolewa kila siku kwa angalau asilimia 43 ya wakazi wa Gaza, iwe bure au kwa bei ya chini sana (chini ya dola moja kwa kifurushi cha kilo 2), na misaada ya unga ya kila mwezi imewafikia watu wapatao milioni 1.2.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Palestina huko Gaza ameripoti kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Amjad Al-Shawa, mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, ameziambia duru za habari kwamba hali ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo imekuwa ngumu na ngumu zaidi.