Rais wa Marekani Donald Trump anasema atamteua Kevin Warsh kuwa mwenyekiti anayefuata wa Benki Kuu ya Marekani. Warsh ni gavana wa zamani wa benki hiyo. Trump amekuwa akishinikiza Benki Kuu ya Marekani kupunguza zaidi viwango vya riba.
Trump alitoa tangazo hilo kwenye mitandao ya kijamii Januari 30. Alisema kwamba Warsh anaweza kuwa mmoja wa wenyeviti “bora” kuwahi kutokea na “hatakuangusha kamwe.”
Kufuatia chapisho hilo, aliwaambia wanabari: “Ningesema kwamba huyu alikuwa mgombea sahihi. Hili halikuwa jambo la kushangaza au kitu kingine chochote. Huyu alikuwa mtu aliyehitimu zaidi, mwanafunzi bora, shule bora, kila kitu kilikuwa, kama, sahihi.”
Warsh, mwenye umri wa miaka 55, alihudumu kama msaidizi maalum wa sera za kiuchumi chini ya Rais George W. Bush kuanzia mwaka 2002. Alikuwa gavana mdogo zaidi katika historia ya benki kuu mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 35 tu, na alichukua jukumu katika kukabiliana na mgogoro wa kifedha duniani.
Yeye ni mhitimu wa Shule ya Sheria ya Harvard na ameshika nafasi za juu katika Morgan Stanley. Kwa sasa anahudumu kama mgeni mashuhuri katika Taasisi ya Hoover ya Chuo Kikuu cha Stanford.
Uteuzi wake unahitaji kuidhinishwa na wabunge kabla ya kuchukua nafasi ya Jerome Powell, ambaye muhula wake unaisha mwezi Mei.
Warsh hivi karibuni amekuwa akielezea msimamo mzuri zaidi kuhusu kupunguzwa kwa viwango. Hata hivyo, Benki Kuu hiyo ya Marekani inaweka sera yake kwa kura nyingi za wanachama wote 12, na bado haijulikani wazi kama maoni yake yatapata uungwaji mkono mkubwa hivyo.