
Kamishna mwenye dhamana na suala la uhamiaji katika Umoja wa Ulaya Magnus Brunner ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA kwamba hali nchini Syria haijaimarika vya kutosha kuruhusu nchi za Umoja wa Ulaya kuanza kuwarudisha kwa wingi Wasyria waliotafuta hifadhi katika mataifa yao. Amesema kwa sasa wanashughulikia kutoa usaidizi kwa lengo la kuboresha hali na kubadilisha hilo pamoja na kwamba wamepewa taarifa na wakala wa waomba hifadhi wa umoja huo kwamba hali nchini Syria inaimarika. Zaidi ya Wasyria 940,000 wanaishi nchini Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Nje, Johann Wadephul, mwanachama wa chama cha kihafidhina cha Kansela Friedrich Merz, CDU, alikumbana na ukosoaji mkali ndani ya chama hicho mwezi Oktoba baada ya kueleza mashaka yake wakati wa ziara ya Syria kuhusu uwezekano wa idadi kubwa ya Wasyria kurudi kwa hiari.