Iringa. Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu Mafinga (FWITC) wamesema wamejipanga kuongeza ubunifu na ujuzi wa kisasa ili kushindana katika soko la thamani la kimataifa badala ya kuwa watumiaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Wanafunzi hao wamesema Januari 30, Mafinga wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya FWITC na Mradi wa FORLAND, ambapo lengo ni kuimarisha mafunzo ya vitendo, matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta ya misitu.

Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao, walisema makubaliano hayo yamefungua fursa mpya za kujifunza uzalishaji wa kisasa na kuongeza thamani ya bidhaa za misitu ili ziweze kushindana katika soko la dunia.

Mwanafunzi wa chuo hicho, Rahabu Msigala, amesema wanafunzi wana ndoto za kufanikiwa kimataifa na wako tayari kubadilika kwa kujifunza teknolojia mpya zitakazowawezesha kuzalisha bidhaa bora, kama ambavyo wanajifunza sasa.

“Tunahitaji msaada wa teknolojia na mitaji; tunawaomba msitupe ndoano bila chambo, na tupo tayari kujifunza na kuzalisha bidhaa zitakazoshindana na za kimataifa,” amesema Rahabu.

Kwa upande wake, mwanafunzi mwingine wa FWITC, Yusuf Nyeho, amesema wamejipanga kupambana na ushindani wa bidhaa kutoka China kwa kuzingatia ubora, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa.

“Tunalenga kuzalisha bidhaa kama makabati, meza, stuli na fanicha nyingine zenye ubora wa kimataifa,” amesema Nyeho, huku akiongeza kuwa,
“Hatutashindana kwa bei pekee, bali kwa ubunifu, uimara na thamani ya bidhaa.”

Nyeho ameongeza kuwa kupitia mafunzo ya vitendo wanayopata chuoni, wanajifunza uzalishaji unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu RAS wa Mkoa wa Iringa, Elias Luvanda, amesema FWITC ni taasisi ya kimkakati kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla, hasa katika kukuza sekta ya misitu.

“Ni wazi kuwa vijana wakipewa ujuzi sahihi na vifaa vya kisasa, wanaweza kubadilisha mwelekeo wa soko na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje,” amesema Luvanda.

Luvanda ameeleza kuwa kuna mpango wa kuanzisha kituo maalumu cha ujuzi wa misitu kitakachowasaidia vijana kupata maarifa ya kisasa na kukuza ubunifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha FWITC, Berthan Odelo, amesema chuo kimeanza kuboresha mitaala yake ili iendane na mahitaji ya soko la dunia kwa kusisitiza zaidi mafunzo ya vitendo.

Berthan amesema ushirikiano na FORLAND utaimarisha matumizi ya teknolojia na ubunifu na kuhakikisha wanafunzi wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko.

Aidha, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa FORLAND, Michael Hawkes, amesema MoU hiyo ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kujenga uwezo wa ushindani wa kimataifa kupitia teknolojia.

Pia, Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti wa FWITC, Dk. Edward Kohi, amesema makubaliano hayo si ya karatasi bali ni mpango wa kubadilisha uwezo wa vijana na kuwafanya wabunifu na wazalishaji.

Vilevile, ushuhuda wa mjasiriamali wa ndani, Method Mgaya, unaonesha manufaa ya mafunzo hayo, akisema FWITC imemsaidia kupata maarifa yaliyomwezesha kuanzisha teknolojia ya finger joint na kushindana na bidhaa za nje.

Hata hivyo, Mgaya amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa mashine na teknolojia za kisasa ili wazalishaji wa ndani waweze kushindana kikamilifu katika soko la kimataifa.

Kwa upande wa sekta binafsi, Martha Haule wa Green Resources Makambako amesema kampuni yao inashirikiana na FWITC kutoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu mnyororo wa thamani wa misitu ili kuwafikisha vijana hao katika mafanikio.

Washiriki wa hafla hiyo walitembelea miundombinu ya chuo, huku viongozi wakisisitiza kuwa itaendelezwa zaidi ili kuendana na mahitaji ya soko la dunia.

Kwa ujumla, wadau wamesema makubaliano kati ya FORLAND na FWITC yamefungua ukurasa mpya wa ushindani wa kimataifa na kuonesha kuwa wanafunzi wa Tanzania wameanza kujipanga kuwa wazalishaji wabunifu katika soko la thamani la dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *