Ajali hiyo ilitokea Jumatano katika migodi ya Rubaya, ambayo inadhibitiwa na waasi wa M23, alisema Lumumba Kambere Muyisa, msemaji wa gavana wa Kivu Kaskazini aliyeteuliwa na waasi, alipozungumza na shirika la habari la Associated Press. Alisema maporomoko ya ardhi yalisababishwa na mvua kubwa.

“Hadi sasa kuna zaidi ya watu 200 waliokufa, baadhi yao bado wako kwenye matope na hawajapatikana,” alisema Muyisa. Aliongeza kuwa watu wengine kadhaa walijeruhiwa na kupelekwa katika vituo vitatu vya afya katika mji wa Rubaya, huku magari ya kubeba wagonjwa yakitarajiwa kuwahamisha majeruhi Jumamosi hadi Goma, jiji lililo karibu zaidi umbali wa takribani kilomita 50.

Gavana wa Kivu Kaskazini aliyeteuliwa na waasi amesitisha kwa muda uchimbaji wa madini kwa njia ya kienyeji katika eneo hilo na kuamuru wakazi waliokuwa wamejenga makazi karibu na mgodi wahamishwe, alisema Muyisa.

“Watu huchimba kila mahali, bila udhibiti au hatua za usalama”

Wachimba migodi katika mgodi wa madini ya Coltan mjini Rubaya, Kivu Kaskazini
Wachimba migodi katika mgodi wa madini ya Coltan mjini Rubaya, Kivu KaskaziniPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mchimbaji madini wa zamani katika eneo hilo aliambia Associated Press kwamba kumekuwa na maporomoko ya ardhi mara kwa mara kwa sababu mashimo huchimbwa kwa mikono, hayajengeki vizuri, na hayafanyiwi matengenezo.

“Watu huchimba kila mahali, bila udhibiti au hatua za usalama. Katika shimo moja wanaweza kuwepo wachimbaji hadi 500, na kwa kuwa vishimo vinakwenda sambamba, shimo moja likiporomoka linaweza kuathiri mengine mengi kwa wakati mmoja,” alisema Clovis Mafare.

Mji wa Rubaya uko katika mtaa wa Masisi, jimboni KIvu Kaskazini, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini katika taifa hilo la Afrika ya Kati ambalo kwa miongo mingi limekuwa likikumbwa na machafuko kutoka kwa majeshi ya serikali na makundi mbalimbali ya waasi, yakiwemo M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao kuibuka kwao upya kumeongeza mapigano na kuzidisha mgogoro wa kibinadamu ambao tayari ulikuwa mbaya.

Kongo ni mmoja wa wasambazaji wakuu wa madini ya koltani, aina ya madini meusi yenye metali adimu ya tantalum, kiungo muhimu katika utengenezaji wa simu janja, kompyuta na injini za ndege.

Nchi hiyo ilizalisha takriban asilimia 40 ya koltani duniani mwaka 2023, kwa mujibu wa Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, huku Australia, Kanada na Brazil zikiwa wasambazaji wengine wakubwa.

Zaidi ya asilimia 15 ya usambazaji wa tantalum duniani unatoka katika migodi ya Rubaya.

Masaibu yasiokwisha ya raia wa mashariki mwa Kongo

Mji wa Rubaya unadhibitiwa na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo toka mwaka 2024
Mji wa Rubaya unadhibitiwa na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo toka mwaka 2024Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mnamo Mei 2024, M23 iliuteka mji huo na kuchukua udhibiti wa migodi yake. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, tangu walipouteka Rubaya, waasi wamekuwa wakitoza kodi katika biashara na usafirishaji wa madini ya koltani, na kuzalisha angalau dola 800,000 kwa mwezi.

Mashariki mwa Kongo imekuwa ikikumbwa na misururu ya migogoro kwa miongo kadhaa. Mapigano mbalimbali yamesababisha moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ikiwa na zaidi ya watu milioni 7 waliokimbia makazi yao, wakiwemo zaidi ya 300,000 waliokimbia tangu Desemba.

Licha ya kutiwa saini kwa makubaliano kati ya serikali za Kongo na Rwanda yaliyosimamiwa na Marekani, na mazungumzo yanayoendelea kati ya waasi na serikali ya Kongo, mapigano bado yanaendelea katika maeneo kadhaa mashariki mwa nchi, yakiendelea kusababisha vifo vingi vya raia na wanajeshi.

Makubaliano kati ya Kongo na Rwanda pia yanafungua njia ya upatikanaji wa madini muhimu kwa serikali ya Marekani na kampuni za Kimarekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *