
Lumumba Kambere Muyisa, msemaji wa gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini aliye chini ya waasi wa M23, aliiambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba ajali hiyo ilitokea Jumatano katika migodi ya Rubaya,mtaani Masisi, ambao unadhibitiwa na kundi la waasi wa M23. Alisema maporomoko hayo yalisababishwa na mvua kubwa.Aliongeza kuwa wengine kadhaa walijeruhiwa na kupelekwa katika vituo vitatu vya afya katika mji wa Rubaya, huku magari ya wagonjwa yakitarajiwa kuwahamisha majeruhi Jumamosi hii kwenda Goma, jiji la karibu takribani kilomita 50 kutoka hapo kwa matibabu zaidi.Mei 2024, kundi la M23 liliteka eneo hilo na kudhibiti migodi yake. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, tangu lilipotwaa Rubaya, waasi hao wamekuwa wakitoza kodi kwenye biashara na usafirishaji wa coltan, na kujipatia angalau dola 800,000 kwa mwezi.