Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya udharura wa kuheshimiana pande mbili katika mazungumzo ya Iran na Marekani.

Abbas Araghchi amesema hayo mjini Ankara Uturuki katika mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan.

Pamoja na masuala mengine, wawaili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusiana na uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda na kimataifa.

Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, huku akiishukuru Uturuki kwa msimamo wake wa kuunga mkono uhuru na mamlaka ya kitaifa ya Iran, alisisitiza msimamo wa Tehran wenye misingi na kusema kwamba Iran haiipi mgongo diplomasia, kwa sharti kwamba, mazungumzo yajengeke katika msingi wa kuheshimiana na kukubali maslahi halali ya Iran.

Akielezea matukio ya ndani ya hivi karibuni nchini Iran, Araqchi alisisitiza umuhimu wa eneo hili kuwa macho dhidi ya simulizi za upande mmoja za vyombo vya habari vya Magharibi-Kiebrania.

Katika mazungumzo hayo, Rais Erdogan, akizungumzia mashauriano ya Ankara ili kupunguza mvutano, ameitaja diplomasia kama suluhisho pekee la suala la nyuklia la Iran na kutangaza utayari wa Uturuki kwa upatanishi wowote. Rais wa Uturuki ameeleza kwamba, ana matumaini Iran itashinda changamoto zilizopo kwa umoja wa kitaifa.

Pande hizo mbili pia zilisisitiza haja ya ushirikiano wa Kiislamu ili kukabiliana na sera za kupenda kuujitanua za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari huko Ankara, Uturuki akiwa pamoja na mwenyeji wake, Hakan Fidan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: Iran iko tayari kuingia katika mazungumzo ya nyuklia ikiwa yatafanyika kwa usawa, kwa kuzingatia maslahi ya pande zote na kuheshimiana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *