Klabu ya Chelsea huenda ikakumbana na pigo katika safari yake ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miongoni mwa kanuni za UEFA kuiondolea faida timu hiyo kucheza kwenye dimba lake la nyumbani katika hatua ya 16 bora.

The Blues walifuzu hatua hiyo baada ya ushindi wa mabao 3-2 ugenini dhidi ya Napoli Jumatano usiku. Hata hivyo, huenda wasiutumie uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge katika mchezo wa marudiano wa 16 bora.

Kwa mujibu wa kanuni za UEFA, mechi zaidi ya moja hairuhusiwi kuchezwa katika jiji moja, au majiji yaliyo ndani ya umbali wa maili 30, katika siku moja ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Lengo la kanuni hiyo ni kuhakikisha usalama wa kutosha bila kuathiri uwezo wa vyombo vya ulinzi.

Mwonekano wa usiku nje ya Uwanja wa Chelsea, Stamford Bridge uliopo jijini London. Picha na Mtandao

Kwa kuwa Arsenal na Tottenham zilimaliza nafasi ya juu kuliko Chelsea katika msimamo wa ligi ya UEFA, timu hizo mbili zitapewa kipaumbele cha kucheza mechi zao za nyumbani siku za Jumanne na Jumatano, Machi 17 na 18. Hali hiyo inaweza kuilazimisha Chelsea kutafuta uwanja mwingine kwa mechi yao ya nyumbani.

Kwa mujibu wa kanuni za UEFA, timu iliyomaliza nafasi ya chini katika hatua ya makundi ndiyo hulazimika kucheza kwenye uwanja mbadala.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa Chelsea kuomba ombi maalumu kwa UEFA ili iruhusiwe kucheza Stamford Bridge, jambo ambalo pia lingehitaji ridhaa ya mamlaka za usalama jijini London.

Mwonekano wa Uwanja wa Chelsea, Stamford Bridge uliopo jijini London. Picha na Mtandao

Kwa kuzingatia kuwa mechi nyingi za soka huchezwa London siku moja mwishoni mwa wiki, suala la usalama halionekani kuwa kikwazo kikubwa.

Njia nyingine kwa Chelsea ni kuomba kucheza Alhamisi, nje ya ratiba ya kawaida ya Jumanne na Jumatano ya Ligi ya Mabingwa, lakini hilo lingeathiri ratiba za waandaaji wa vipindi vya televisheni ambao huenda wasikubali mabadiliko hayo.

Katika taarifa yao, UEFA wamesema:

“Majadiliano kuhusu ratiba yanaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za eneo husika kutokana na migongano ya michezo katika miji, ikiwemo mechi zitakazochezwa Machi.”

Chelsea itachuana na moja ya timu za Monaco, Qarabag, Newcastle au PSG katika hatua ya 16 bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *