
Dar/Zanzibar. Klabu tatu za Tanzania leo zitakuwa na mechi muhimu katika viwanja na miji tofautiilizoshikilia hatima zao kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika msimu huu.
Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba itakuwa ikianza kupanda mlima mrefu wa kujaribu kufanya maajabu ya kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapoikaribisha, Esperance ya Tunisia.
Matokeo yoyote tofauti na ushindi katika mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni yatamaanisha kuwa safari ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itakuwa imefikia tamati.
Lakini kama itapata ushindi, angalau Simba itabaki na matumaini ya kuingia hatua inayofuata lakini pia italazimika kupata ushindi katika mechi mbili zitakazobakia huku pia ikihitajika kuombea matokeo ya timu nyingine yawe yenye faida kwa upande wao.
Ukiweka kando hitajio la ushindi wa kwanza kwa Simba kwenye hatua hiyo, kuvuna pointi tatu leo kutaifanya ilipe kisasi cha kupoteza kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza baina yao, uliochezwa Jumamosi, Januari 24, 2026.
Mechi hiyo itachezeshwa na refa Celso Alvacao kutoka Msumbiji ambaye wasaidizi wake ni Zacarias Baloi na Venestancio Cossa huku mwamuzi wa nne akiwa ni Simoes Guambe, wote wakiwa wanatoka Msumbiji.
Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa na nguvu mpya ya nyota sita wa kigeni ambao imewasajili katika dirisha dogo la usajili ambao ni Jospin Loemba, Libasse Gueye, Anicet Oura, Clatous Chama, Djibrilla Kassali na Ismael Toure.
Kocha wa Simba, Steve Barler amesema kuwa msimamo wa kundi lao ulivyo, unawalazimisha kupata ushindi leo vinginevyo watakuwa wanaaga mashindano hayo.
“Tunajua kwamba tunacheza dhidi ya timu nzuri. Tunaamini kwamba bado nafasi yetu ipo ya kusonga mbele ukizingatia tutakuwa nyumbani na tutakuwa na sapoti ya mashabiki wetu.
“Ili tupate ushindi tunatakiwa kuimarika hasa katika kutumia nafasi. Tunatakiwa kutengeneza sana nafasi na tunafahamu kwamba katika Ligi ya Mabingwa Afrika huwa hakuna timu rahisi,” alisema Barker.
Azam yasaka muendelezo
Baada ya kuibuka na ushindi katika mchezo uliopita ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Nairobi United, Azam FC leo italazimika kuhakikisha inarudia kile ilichokifanya Kenya wakati timu hizo zitakaporudiana katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 1:00 usiku.
Ushindi wa leo utaiweka Azam katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali kwani itafiki9sha pointi sita ambazo Maniema ya DR Congo inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi lao B inazo hadi sasa.
Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Nairobi United unaonekana unaweza kuipa faida Azam FC iwapo wachezaji wake watautumia vyema kuhakikisha wawakilishi hao wa Tanzania wanapata ushindi leo.
Katika mechi tatu zilizopita za Kombe la Shirikisho Afrika, Nairobi United imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita ikiwa ni wastani wa kufungwa mabao mawili katika kila mchezo.
Refa wa mechi hiyo atakuwa ni Gerson Angono kutoka Guinea ya Ikweta.
Atezambong Carine kutoka Cameroon atakuwa msaidizi namba moja na Juan Ngua Eleng atakuwa msaidizi namba mbli hukuWilly Ngah kutoka Cameroon akiwa refa wa akiba.
Singida BS ishindwe yenyewe
Singida Black Stars itaanza kunusa hatua ya robo fainali ikiwa itaibuka na ushindi ugenini katika Uwanja wa Alphonse Massemba-Debat (Brazzaville) dhidi ya wenyeji wao AS Otoho ya huko Congo.
Ushindi utaifanya Singida Black Stars ifikishe pointi saba na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi C pasipo kutegemea matokeo ya mchezo baina ya Stellenbosch na CR Belouizdad.
Kundi hilo kwa sasa linaongozwa na CR Belouizdad yenye pointi sita ikifuatiwa na Stellenbosch yenye pointi nne huku Singida Black Stars ikiwa nafasi ya tatu na mkiani wapo Otoho wenye pointi