Waziri Mkuu wa Japani, Takaichi Sanae, na mwenzake wa Uingereza, Keir Starmer, wamekubaliana kushirikiana kwa karibu na nchi zenye mtazamo unaofanana ili kuimarisha minyororo ya usambazaji wa madini muhimu.
Takaichi na Starmer anayezuru Japani walizungumza kwa takribani dakika 20 katika ofisi ya waziri mkuu huko Tokyo Januari 31 jioni baada ya kupokea salamu kutoka kwa Kikosi cha Kujihami cha Japani.
Katika upande wa usalama, viongozi hao wawili walikubaliana kukuza kimkakati ushirikiano katika usalama wa mtandao, kuharakisha maendeleo ya pamoja ya pande tatu na Italia ya ndege ya kivita ya kisasa zaidi na kufanya mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi yanayojulikana kama “wawili kwa wawili” mwaka huu.
Kuhusu uchumi na usalama wa kiuchumi, Takaichi na Starmer walikubaliana kupanua ushirikiano wa viwanda katika nyanja za uzalishaji wa umeme wa upepo, kwanta na nyuklia. Pia walithibitisha hitaji la uratibu miongoni mwa nchi zenye mtazamo unaofanana na za nchi zao kuelekea lengo la kuimarisha minyororo ya usambazaji wa madini muhimu. Hili linakuja wakati kukiwa na wasiwasi unaoongezeka wa kimataifa kuhusu vikwazo vya usafirishaji nje vya China kwenye madini hayo.
Takaichi na Starmer waliendelea kubadilishana maoni kuhusu mada mbalimbali katika chakula cha jioni. Suala la kuhakikisha eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki liliibuliwa kutokana na mkutano wa Starmer na Rais wa China Xi Jinping, kabla ya ziara yake nchini Japani. Hali katika Mashariki ya Kati na Ukraine pia zilijadiliwa.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Takaichi alisema yeye na waziri mkuu wa Uingereza wamekubaliana kuongeza ushirikiano wa pande mbili hadi kiwango kipya na kuuimarisha zaidi. Alisema nchi hizo mbili zitaungana kwa karibu zaidi ili kujenga enzi mpya kwa Japani na Uingereza katika karne ya 21 ambapo jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na migogoro migumu.
Starmer alisema, “Ziara yangu hapa leo inakuja wakati ambapo mitikisiko ya kijiografia, kiuchumi na kiteknolojia inatikisa ulimwengu.” Aliongeza kuwa mwitikio wa nchi hizo mbili lazima uwe “wa nguvu na uwazi.”
Waziri huyo mkuu wa Uingereza alisisitiza umuhimu wa uratibu wa karibu katika kukuza biashara huria. Alisema, “Sote ni mataifa yanayojivunia biashara, kwa hivyo tuna nia ya wazi ya kudumisha biashara huru na inayotabirika na eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki ili kuhakikisha biashara zetu zinaweza kustawi katika ulimwengu wenye misukosuko.”
Starmer alitoa mwaliko kwa Takaichi kutembelea Uingereza mwaka huu.