Barcelona, Hispania. Mke wa Robert Lewandowski, Anna Lewandowski amefichua kuwa mshambuliaji huyo ana uwezekano mkubwa wa kuachana na Barcelona baada ya msimu huu kumalizika.

Mkataba wa Lewandowski (37) na Barcelona utafikia tamati Juni mwaka huu na miezi michache iliyopita, tetesi zilidai kuwa klabu hiyo haina mpango wa kumuongezea mkataba mpya.

Tangu hapo upande wa Lewandowski haukuzungumza chochote juu ya hatima ya mshambuliaji huyo hadi sasa ambapo mkewe ameibuka na kuonyesha muelekeo wa mumewe.

Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski akiwa na mkewe Anna pamoja na watoto wao. Picha na Mtandao

Anna ambaye pia ni mtaalam binafsi wa mazoezi wa Lewandowski amesema kuwa mshambuliaji huyo ana uwezekano finyu wa kuwepo Barcelona msimu ujao.

“Tutaangalia msimu utaendaje ndani ya Barcelona mwaka huu kwa sababu tuseme inaweza kuwa msimu wa mwisho kwa mume wangu hapa.

“Hivyo tunakamua kama limao. Tunafurahia kila nyakati, kila mchezo na mashabiki kwa sababu tunajua kwamba siku moja hatuwezi kuwa na nafasi hiyo.

“Mbele itakuaje? Hatujui lakini hiyo ndio njia ya mchezaji mkubwa na hasa mwanamichezo wa hadhi ya juu na tupo tayari kwa hilo,” amesema Anna.

Kauli ya Anna ambaye amezaa watoto wawili na Lewandowski, hapana shaka itaziweka mkao wa kula klabu mbalimbali kubwa barani kuanza kunyemelea saini yake kwa vile nyota huyo wa Poland anaonekana bado ana makali ya kufumania nyavu hadi sasa.

Msimu huu tayari Lewandowski ameshaifungia Barcelona idadi ya mabao 12 katika michezo 25 huku akiiongoza timu hiyo kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Hispania, kutwaa Kombe la Hispania na pia kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski akiwa pamoja na mke wake, Anna Lewandowski. Picha na Mtandao

Hata hivyo amekuwa hana uhakika wa kuanza katika kikosi cha kwanza cha Barcelona kwa vile Meneja wa timu hiyo, Hans Flick anaonekana kupendelea zaidi kumtumia Ferran Torres.

Kiujumla, mshambulliaji huyo amethibitisha kuwa alistahili kusajiliwa na Barcelona kwani tangu ajiunge nayo mwaka 2022 akitokea Bayern Munich, ameifungia mabao 113 katika mechi 173 za mashindano tofauti alizoichezea.

Lewandowski ni miongoni mwa washambuliaji ambao wamekuwa na muendelezo mzuri wa kufumania nyavu kwa muda mrefu barani Ulaya.

Takwimu zinaonyesha katika mechi 848 alizochezea klabu tano tofauzi kwenye soka la ushindani, amefunga mabao 622 huku akiifungia timu yake ya Taifa ya Poland mabao 88 katika mechi 163.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *