Chombo cha habari cha Iran kimesema mtu mmoja ameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika mlipuko kuliotokea kwenye jengo la makazi kusini mwa nchi hiyo.
Mlipuko huo ulitokea katika jiji la Bandar Abbas Januari 31. Shirika la Habari la Tasnim, ambalo lina uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lilinukuu mamlaka ya zimamoto ikisema mlipuko huo ulisababishwa na uvujaji wa gesi.
Shirika hilo la habari lilikanusha madai kwamba kamanda wa jeshi la wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi alilengwa. Lilisema uvumi huo si wa kweli kabisa na ni sehemu ya operesheni za kisaikolojia zinazofanywa na makundi yanayoipinga Iran.
Kando na hilo, watu wanne pia waliripotiwa kuuawa katika mlipuko mwingine wa gesi katika jengo la makazi kwenye mji wa kusini-magharibi wa Ahvaz.
Maandamano makubwa ya kupinga serikali yamesababisha vifo vingi nchini Iran. Rais wa Marekani, Donald Trump, amekuwa akiongeza shinikizo la kijeshi kwa nchi hiyo ili iingie katika mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.