
BAADA ya Mbeya Kwanza kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Jesus Ducapel Moloko, kocha wa timu hiyo, Maka Mwalwisi, amesema wapinzani wajipange vizuri katika raundi hii ya pili kutokana na ubora wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalwisi, amesema usajili wa Moloko umekuja kipindi sahihi kutokana na mahitaji ya timu hiyo kwa sasa, ambayo lengo kubwa ni kuhakikisha kikosi hicho kinarejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2021-2022.
“Hakuna asiyejua ubora na uzoefu wa Moloko, ni mchezaji mzuri sana ambaye kwa timu ya Championship kuipata saini yake ni jambo la kujivunia, nawasifu sana viongozi kwa kuniongezea mtu ninayeona atawasumbua sana wapinzani,” amesema Mwalwisi.
Nyota huyo aliyewahi kuitumikia Yanga kuanzia Agosti 13, 2021 hadi Januari 28, 2024, wakati alipojiunga na kikosi hicho akitokea AS Vita ya kwao DR Congo, ambapo kwa sasa amejiunga na Mbeya Kwanza baada ya kuachana na AS Kigali ya Rwanda.
Moloko alijiunga na AS Kigali Agosti 28, 2025, baada ya kuachana na ES Mostaganem ya Algeria, ingawa hakudumu nayo baada ya kuondoka Januari 2026, huku akichezea timu mbalimbali zikiwemo za Diyala SC ya Iraq na Al Sadaqa Shahat SC ya Libya.
Nyota huyo amejiunga na timu hiyo ambayo msimu huu hadi sasa kabla ya mechi ya jana Jumapili dhidi ya Mbuni FC ya jijini Arusha, iko nafasi ya tatu na pointi 34, baada ya kushinda mechi 11, ikitoka sare moja tu na kupoteza mitatu kati ya 15.