Jeshi la Walinzi wa Mapindzi ya Kiislamu (IRGC) katika miongo ya hivi karibuni limefanya vyema, hasa katika mapambano dhidi ya magaidi wa kundi la Daesh (ISIS) na pia katika Vita vya Siku 12 na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni taasisi iliyotokana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, limekuwa na nafasi muhimu katika matukio ya kikakanda na usalama wa taifa wa Iran katika kipindi cha miongo mitano ya karibuni. IRGC imefanya vyema hasa katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS na vita vya siku 12 na utawala wa Kizayuni.

Katika suala la Daesh, kuasisiwa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri katika miaka ya 2013 na 2014 na kuenea kwa kasi magaidi wa kundi hilo huko Iraq na Syria kulitishia pakubwa eneo zima la Asia Magharibi. Aghalabu ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kama mchakato wa kusonga mbele Daesh ungeendelea si tu serikali za Iraq na Syria zilikuwa katika mkondo wa kuporomoka, bali wimbi la hali ya mchafukoge lilikuwa likienea katika nchi jirani, ikiwemo Iran. Katika mazingira hayo Iran ilitangaza kuwa ilitoa ushauri wa kijeshi, mafunzo kwa vikosi vya majeshi ya Iraq na Syria na msaada wa ushauri kwa ombi la serikali za nchi hizo. Jeshi la IRGC, hasa Kikosi cha Quds, kilikuwa mhimili muhimu wa shughuli zote hizo. 

Huko Iraq, baada ya kusonga mbele ghafla Daesh na kuuteka mji wa Mosul mwaka 2014, muundo wa ulinzi wa nchi hiyo uliathirika pakubwa. Ripoti nyingi zinaonyesha kuwa Iran ilikuwa na mchango na nafasi muhimu katika kuimarisha safu za ulinzi za Baghdad, Samarra na Karbala kwa kutuma washauri wa kijeshi na kusaidia kupanga kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq kwa jina la al Hashdu Shaabi. Aghalabu ya makamanda wa Kiiraqi wamekiri katika mahojiano kwamba mafunzo yaliyotolewa na washauri wa Kiirani yalikuwa na taathira kubwa katika kuzidisha uwezo wa makabiliano wa vikosi vya jeshi la Iraq. Pia uratibu kati ya vikosi vya Iraq na makundi ya wapiganaji ya ndani katika vita dhidi ya Daesh ulikuwa sehemu ya shughuli ambazo, ambapo kwa mujibu wa vyanzo rasmi vya Iraq, zilifanywa kwa ushauri wa Iran. Hasa ushiriki chanya na madhubuti wa  Jenerali Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC, na muongozo wake vilikuwa na nafasi kuu katika kusambaratisha sehemu kubwa ya wanamgambo na zana za kundi hilo la kigaidi na hatimaye kushindwa kikamilifu Daesh huko Iraq.  

Wapiganaji wa kundi la Daesh

Huko Syria pia hali ilikuwa sawa na hiyo. Serikali ya Syria baada ya kuanza machafuko mwaka 2011, katika miaka ya mwanzoni mwa mgogoro nchini humo ilikuwa imepoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo. Iran ilitangaza kuwa inatoa misaada ya ushauri kufuutia ombi la serikali ya Syria sambamba na kusonga mbele Daesh mashariki mwa nchi hiyo na kutishia mji wa Damascus. Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa ushirikiano huo ulisaidia kuzuia kuanguka Damascus na kukombolea maeneo muhimu ya Syria yaliyokuwa mikononi mwa kundi la Daesh. Washauri wa jeshi la IRGC walikuwa na mchango na nafasi kuu katika oparesheni kama za kukomboa miji muhimu ya Syria kama Halab na Bukamal. 

Pamoja na hatua zote hizo, moja ya nukta muhimu ni mchango wa Iran katika kuasisiwa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Syria wenyewe na pia kuanzishwa vitengo vya mapambano kama vile makundi ya Zainabiyyun, Fatimiyyun na Haydariyyun, pamoja na kushiriki harakati ya Hizbullah ya Lebanon ambayo ilikuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya Daesh.  Wanamapambano hao waliweza kutengeneza ngome imara na kuzuia kusonga mbele Daesh na kisha kufanikiwa hatua kwa hatua kuwafurusha magaidi wa kundi hilo. Suala hili pia limebainishwa katika ripoti za vituo vya kimataifa vya utafiti, kwamba ushirikiano kati ya vikosi vya jeshi la Syria na msaada wa ushauri wa kigeni ulikuwa moja ya sababu kuu za kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika miaka iliyofuata. Hatimaye Kamanda Shahidi Qassem Soleimani mwishoni mwa Novemba mwaka 2017 alimwandikia barua Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akitangaza kupata kipigo cha mwisho kundi la Daesh baada ya kukombolewa mji wa Bukamal huko Syria. 

Jenerali Qassem Soleimani

Katika Vita vya Siku 12 mwaka jana ambavyo vimetajwa kuwa moja ya makabiliano makali zaidi ya moja kwa moja kati ya Iran na utawala wa Kizayuni wa Israel, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilikuwa na nafasi kuu katika majibu ya kijeshi ya Iran. Vita hivyo vilianza baada ya mivutano ya kiusalama na mashambulizi ya mjibizano na kufikia katika kiwango kikubwa cha mashambulizi ya anga, ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni). Weledi wa mambo katika kanda hii wanaamini kuwa mapigano hayo yalikuwa hatua muhimu katika kudhihirisha uwezo wa Iran wa kukabiliana na mashambulizi ya adui na nafasi ya kikosi cha anga cha jeshi la IRGC.  

Katika uga wa makombora, kikosi cha anga cha IRGC kilifanya msururu wa mashambulizi yaliyolenga shabaha kwa usahihi, ya tabaka mbalimbali na kuvurumisha makombora zaidi ya 500 dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Israel. Ripoti zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya kikanda na kimataifa zilionyesha kuwa IRGC ilitumia mchanganyiko wa makombora ya balistiki ya masafa ya kati na yale yanayorushwa kupiga shabaha maalumu. Mchanganyiko wa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani, kama wanavyosema wachambuzi wa mambo, uliweka muundo wa ulinzi wa Israel katika hali ya mmomonyoko na kuonyesha kwamba IRGC ina uwezo wa kutengeneza mashinikizo endelevu na yenye ufanisi dhidi ya adui Mzayuni katika vita vya pande kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *