Maafisa wa utalii nchini Japani na Korea Kusini wametoa data zinazoonyesha kwamba idadi ya wasafiri kati ya nchi hizo mbili ilifikia kiwango cha juu zaidi mwaka 2025.

Shirika la Utalii la Korea lilitangaza Januari 30 kwamba wasafiri wapatao milioni 3.65 wa Japani walitembelea Korea Kusini mwaka jana. Idadi hiyo ilikuwa ongezeko la zaidi ya wasafiri 400,000 kutoka mwaka uliotangulia.

Shirika la Kitaifa la Utalii la Japani linakadiria kwamba raia wa Korea Kusini zaidi ya milioni 9.45 walitembelea Japani katika kipindi hicho hicho.

Idadi ya wasafiri kati ya mataifa hayo mawili ilizidi milioni 13, na kuweka rekodi mpya.

Idadi inayoongezeka ya watalii wa Korea Kusini ilitembelea sio tu miji mikubwa ya Japani, kama vile Tokyo na Osaka, lakini pia maeneo ya ndani kwa chemchemi za maji moto au gofu.

Korea Kusini ilisalia kuwa kivutio maarufu zaidi kwa wasafiri wa Japani, haswa vizazi vichanga, ambavyo vinapenda tamthilia na muziki wa K-POP wa Korea Kusini.

Zaidi ya hayo, makampuni ya ndege yameongeza safari za ndege za kawaida kati ya miji ya Japani na Korea Kusini katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo mwezi Machi, safari ya kwanza ya kawaida kati ya Shizuoka nchini Japani na Busan nchini Korea Kusini inatarajiwa kuanza.

Kuboresha mahusiano ya pande mbili kunaonekana kuliwatia moyo Wajapani na Wakorea Kusini kutembeleana, wakati huu ambapo idadi ya watalii wa China nchini Japani imepungua kutokana na uhusiano unaozorota kati ya Japani na China.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *