Amesema hayo jijini Dar es salaam nchini Tanzania wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Afrika wa Mkakati wa Taifa wa Umechanishaji wa Kilimo wa Tanzania 2026–2036 katika ufunguzi wa Mkutano wa Afrika kuhusu utumiaji endelevu wa mashine kwenye sekta ya kilimo.
Ufunguzi umeanda sanjari na uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Utumiaji wa mashine kwenye kilimo nchini Tanzania mwaka 2026-2036.
Beth Bechdol, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO akizungumza kwenye mkutano huo jijini Dar es salaam, Tanzania.
Mashine bila mafunzo ya matumizi haileti maana – Bechdol
“Kuleta mashine kubwa bila ufadhili, mafunzo, huduma za matengenezo au kulingana na mazingira ya ndani hakujaleta matokeo ya kudumu. Afrika haihitaji tena vifaa vinavyokaa bila kutumika. Inahitaji mifumo inayofanya kazi,” amesema Bi. Bechdol.
“FAO tunaona kuwa uwepo endelevu wa mashine za kisasa kwenye sekta ya kilimo ni kichocheo cha mageuzi—sio mashine kuchukua nafasi ya watu, bali zana zinazowawezesha watu, kupunguza kazi nzito na kuwapa wanawake nafasi ya kulima kwa tija zaidi,” ameongeza Bi Bechdol.
Ili kufanikisha mabadiliko haya, amesema, kunahitajika suluhu zinazoongozwa na ushahidi, uzalishaji na mifumo ya huduma ya ndani iliyo imara, mifumo bunifu ya ufadhili, sera wezeshi, na—zaidi ya yote—ushirikiano.
Mashine kwenye sekta ya kilimo ni hitaji la kimkakati
Akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema matumizi ya mashine kwenye sekta ya kilimo ni hitaji la kimkakati: “kupitia vitendo, tunaweza kubadilisha kilimo cha Afrika kiwe sekta iliyo na matumizi endelevu ya mashine kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.”
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya FAO, serikali ya Tanzania na unakutanisha wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, watafiti, washirika wa maendeleo, vijana na wakulima ili kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kubaini suluhu zinazoweza kupanuliwa kwa ajili ya kuendeleza matumizi endelevu ya mashine kwenye sekta ya kilimo barani Afrika.
Mkakati wa Tanzania umeoanisha Mfumo wa FAO–Muungano wa Afrika wa Matumizi endelevu ya mashine kwenye kilimo barani Afrika, (F-SAMA) na unahakikisha kuwa wanawake na vijana wako katikati ya mabadiliko.
Pengo la mashine kwenye sekta ya kilimo barani Afrika
Afrika inaendelea kubaki nyuma ikilinganishwa na maeneo mengine katika matumizi ya mashine za kisasa shambani. Wakati sehemu kubwa ya Asia na Mashariki ya Karibea zilipanua kwa kasi matumizi ya matrekta, wakulima wengi barani Afrika bado wanategemea jembe la mkono au wanyama.
Jitihada za awali za matumizi ya mashine mara nyingi zilikwama kwa sababu vifaa havikufaa mifumo ya wakulima wadogo na havikuungwa mkono na minyororo ya usambazaji ya ndani kwa ajili ya matengenezo, vipuri na ukarabati.
Mkutano unaendelea hadi tarehe 6 Februari.
Soma kwa kina taarifa hiyo hapa.