
Dar es Salaam. Kampuni ya Altezza Travel imetajwa kuwa Kampuni Bora ya Utalii katika Kanda ya Kaskazini kwenye tuzo za kwanza za Serengeti Awards, hatua inayoiweka kampuni hiyo miongoni mwa wadau wenye ushawishi mkubwa katika sekta ya utalii nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla maalum iliyofanyika Jumamosi, Januari 31, 2026 chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, huku Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akiongoza hafla hiyo.
Tuzo za Serengeti zilizozinduliwa mwaka huu na wizara, zinalenga kutambua ubora, ubunifu na uwajibikaji wa kibiashara katika sekta ya utalii ambayo inaendelea kukua kwa kasi nchini Tanzania.
Kupitia tuzo hizo, waendeshaji wa utalii wa ndani wanapimwa kwa viwango vya kimataifa, huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye ubora wa huduma, uhifadhi wa mazingira na uwajibikaji kwa jamii.
Kushinda katika kipengele cha Kanda ya Kaskazini kunachukuliwa kuwa moja ya heshima kubwa zaidi katika sekta hiyo, kutokana na kanda hiyo kuchangia takribani asilimia 85 ya watalii wa kimataifa wanaoingia nchini pamoja na mapato ya utalii.
Kanda hiyo pia inajumuisha vivutio vikuu vya utalii barani Afrika ambavyo ni Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Bonde la Ngorongoro — maeneo yanayofanya ushindani miongoni mwa kampuni za utalii kuwa mkubwa zaidi.
Kwa kutwaa nafasi ya juu, Altezza Travel imejipambanua kama kinara katika eneo linaloonekana kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa utalii nchini.
Tuzo hiyo inakuja mwishoni mwa mwaka wenye mafanikio makubwa kwa kampuni hiyo. Mwaka 2025, Altezza Travel iliweka historia kwa kuwa kampuni ya kwanza ya utalii Tanzania kupata vyeti vya kimataifa vya B Corp na Travelife Certification, vinavyopima mchango wa kampuni kwa jamii, utunzaji wa mazingira, uwazi na uendeshaji bora.
Aidha, kampuni hiyo ilitajwa kuwa Leading Tour Operator in Tanzania kwenye tuzo za kimataifa za World Tourism Awards na pia kutambuliwa kama mlipa kodi mkubwa zaidi katika Mkoa wa Kilimanjaro, jambo linaloonyesha mchango wake wa kiuchumi kwa jamii inayozunguka shughuli zake.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa Miradi wa Altezza Travel, Dickson Muganda, alisema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa kwa watu.
“Watu ndio msingi wa kila tunachokifanya. Tunawekeza sana kwa timu yetu, na tuzo pamoja na vyeti hivi vinaakisi kujituma na taaluma yao,” alisema Muganda.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiweka mkazo katika kukuza vipaji vya vijana kupitia programu maalum za mafunzo ya vitendo yenye malipo, ambapo wengi wa washiriki huajiriwa rasmi baada ya mafunzo.
“Tunajivunia kuwa kazi yetu siyo tu kuhusu utalii, bali pia kuchangia safari ya Tanzania kuelekea kuwa taifa la kisasa na la viwanda,” alisema.
Maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii walisema kuanzishwa kwa Serengeti Awards ni sehemu ya mabadiliko ya kimkakati yanayolenga kukuza utalii endelevu na wenye thamani kubwa, badala ya utalii wa wingi usiozingatia ubora.
Wizara ina matumaini kuwa utambuzi wa kampuni kama Altezza Travel utahamasisha waendeshaji wengine kuboresha masuala ya ajira, uhifadhi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka maeneo ya utalii.
Wachambuzi wa sekta ya utalii wanasema tuzo hizo zinatarajiwa kuongeza ushindani chanya miongoni mwa kampuni, hali itakayochochea maboresho katika utoaji huduma, mazingira ya kazi na miradi ya uendelevu.
Mbali na heshima, mpango huo unatarajiwa kuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wafanyakazi na jamii kwa ujumla kwa kuhimiza mishahara yenye staha, uendeshaji wa kimaadili na maendeleo ya utalii yanayowajibika.
Wadau wa utalii wanasema wakati Tanzania ikiendelea kujipanga kama moja ya vivutio vinavyoongoza duniani, kampuni kama Altezza Travel zitakuwa na nafasi muhimu katika kuunda mustakabali wa sekta hiyo.