Katika taarifa iliyotolewa leo Februari 3, kutoka mji mkuu Kyiv nchini Ukraine, msaada huo unaoungwa mkono na serikali za Uingereza, Marekani, na Denmark umelenga kampuni za usambazaji maji na mifumo ya kupasha joto wakati nchi hiyo ikikabiliwa na baridi kali ya nyuzi joto 20 chini ya sifuri (-20). 

UNICEF imethibitisha kuwa jenereta nyingine 149 ya uwezo tofauti zitatolewa katika wiki zijazo ili kuimarisha nishati mbadala katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Kukatika kwa umeme msimu wa baridi kali

Hali ya kukatika kwa umeme wakati huu wa msimu wa baridi kali imesababisha mabomba ya maji na yale ya mifumo ya joto kupasuka, jambo linalohatarisha maisha ya raia. Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine, Munir Mammadzade,amesema akisisitiza ukubwa wa tatizo hilo.

“Hivi sasa, watoto na familia zao waanaishi katika hali ya hofu wakiwaza kujiokoa kila wakati.”

Mammadzade amebainisha kuwa wazazi wanapambana sana kuwapatia maji na chakula cha moto watoto wao huku vitalu na hospitali zikitegemea nishati hiyo mbadala ili kubaki wazi.

Ukarabati wa dharura na usalama wa watoto

Msaada huu wa jenereta ni sehemu ya mkakati wa UNICEF wa maandalizi ya msimu wa baridi ambao tayari umewafikia watu milioni 1.2 kupitia ukarabati wa miundombinu na nishati mbadala. UNICEF imeeleza kuwa baridi kali inawaweka watoto katika hatari ya kupata magonjwa ya upumuaji, huku giza likiongeza msongo wa mawazo.

“Jenereta hizi zitawasaidia mafundi ambao ni kama mashujaa katika jamii kuendeleza  mifumo ili kupata joto, hospitali zilizo wazi, na maji yanayotiririka.” Ameongeza Mammadzade.

Hadi sasa, zaidi ya watu 187,000, wakiwemo watoto 88,000, wamepatiwa msaada wa fedha taslimu ili kumudu gharama za maisha wakati huu wa dharura. Usambazaji wa jenereta hizi unasaidia manispaa kurejesha huduma kwa haraka pindi hitilafu zinapotokea na kupunguza muda ambao hospitali na shule zinakaa bila nishati. UNICEF imebainisha kuwa uwekezaji huu ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kijamii inayohudumia familia zilizoathiriwa na vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *