
Paje. Kampuni ya mawasiliano Yas imezindua rasmi duka jipya katika eneo la Paje, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na suluhisho za kidijitali kwa wakazi wa Paje, maeneo ya jirani na Zanzibar kwa ujumla.
Ufunguzi wa duka hili unathibitisha dhamira ya Yas, kusogeza huduma karibu zaidi na jamii na kuendelea kuwa mshirika wa kuaminika wa kidijitali kwa Watanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kusini – Unguja, Ndugu Mbaraka Omar Kasongo, alisema: “Uzinduzi wa duka la Yas hapa Paje ni ishara nzuri ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wilaya yetu. Hii ni fursa kwa wakazi kupata huduma za kisasa za mawasiliano kwa ukaribu zaidi. Tunapongeza uwekezaji huu, tunatarajia faida yake itakuwa kwa wote – jamii, wajasiriamali na sekta ya mawasiliano Zanzibar.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas – Zanzibar, Aziz Said Ali, amesema duka la Paje linaendeleza uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hiyo katika kuboresha ubora wa mtandao na huduma za mawasiliano visiwani humo.
“Tumeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika upanuzi na uboreshaji wa mtandao wetu wa 4G na 5G kote Zanzibar, hatua ambayo imeifanya Yas kuwa mtandao namba moja, unaoaminika na wenye kasi zaidi visiwani Zanzibar. Ufunguzi wa duka hili la Paje ni sehemu ya dhamira yetu ya kuwapa wakazi wa eneo hili na Zanzibar kwa ujumla huduma kwa ukaribu zaidi, urahisi na zenye ubora unaoendana na mahitaji ya sasa ya mawasiliano,” alisema.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas na Mixx, Mwangaza Matotola, alisema duka la Paje linafikisha idadi ya maduka ya Yas Zanzibar kufikia saba, huku maduka zaidi ya 500 yakipatikana nchi nzima.
“Duka hili limejengwa kutokana na mahitaji ya wakazi wa Paje ambao wanahitaji huduma za haraka na zinazopatikana kwa urahisi. Tumelenga kuhakikisha kila mteja anapata msaada wa huduma, ushauri wa kitaalamu na utatuzi wa changamoto kwa ufanisi,” alisema.
Aliongeza kuwa Yas na Mixx zinaendelea kuwahudumia wateja kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupitia nambari 100 ya huduma kwa wateja na majukwaa ya kidijitali ili kutoa msaada unaopatikana wakati wowote.
Katika kipindi hiki ambacho kampuni inasherehekea mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, Yas inaendelea na Kampeni ya Mwaka Mmoja, ambayo inatoa zawadi mbalimbali zikiwemo shilingi milioni moja kila siku, shilingi milioni tano kila wiki, safari kwa washindi kumi kwenda Dubai, na zawadi kuu ya shilingi milioni 100.
Uzinduzi wa duka la Paje ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kusini Unguja, viongozi wa Yas na Mixx, wateja, wadau na waandishi wa habari.