Katika vita vinavyofanyika mbali na macho ya vyombo vya habari, sauti za waasi, watetezi wa haki na raia waliokumbwa na madhara zinaanza kujitokeza.
Kiongozi wa kijeshi wa kundi la waasi la Ukombozi wa Watu wa Oromia, OLA, Jaal Marroo, anaesakwa kwa udi na uvumba na serikali ya Ethiopia, anasema analazimika kuhama mara kwa mara ili kukwepa mashambulizi ya droni.
Marroo, anayejulikana pia kama Kumsa Diriba, anaiongoza OLA kutokea maficho ya misituni katika eneo la Oromia, mkoa mkubwa zaidi nchini Ethiopia wenye wakazi takriban milioni 40.
Serikali imemtaja Marroo, aliyekuwa mwanafunzi, kama gaidi, na kuishutumu OLA kwa kuua raia katika mashambulizi yanayochochewa na chuki za kikabila.
Ukiukaji wa haki za binadamu: Pande zote zalaumiwa
Hata hivyo, katika mahojiano ya nadra aliyotoa kwa shirika la habari la AP akiwa mafichoni pake, Marroo amekana madai hayo.
“Wanajeshi wetu wanafanya kazi kwa nidhamu kali ya kijeshi na dira ya wazi ya kisiasa. Tunakataa na kulaani kitendo chochote kinachowadhuru raia wasio na hatia. Kanuni zetu za maadili zinakataza kulenga raia. Pia tunasisitiza tena kuwa tunakaribisha uchunguzi huru unaofanywa na chombo cha kimataifa kisichoegemea upande wowote.”
OLA imekuwa ikipambana na serikali tangu mwaka 2018, mzozo ambao mara nyingi umefunikwa na migogoro mingine mikubwa ya Ethiopia, ikiwemo vita vya Tigray.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameituhumu OLA kwa mauaji, ubakaji na utekaji nyara, huku mashirika ya haki za binadamu yakisema pia vikosi vya serikali vinahusika katika ukiukwaji mkubwa.
Msemaji wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, Sarah Kimani, anasema utafiti wao unaonyesha raia wamenaswa katikati ya mapigano.
“Utafiti tulioufanya unaiweka OLA na majeshi ya serikali katikati ya mzozo huu kwa kuhusika katika mauaji ya kiholela, mateso, utekaji nyara na ubakaji wa wanawake… makundi yote mawili yamewajibika kwa unyama unaotekelezwa dhidi ya raia katika eneo la Oromia.”
Kwa raia, gharama ya vita ni kubwa. Familia zimeripoti mauaji ya kiholela, vitisho na utekaji nyara. Wengine wanasema kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine ni jambo gumu sana, huku hospitali na vituo vya afya vikishambuliwa au kuharibiwa.
Katika hali hii, baadhi ya vijana wanasema waliona silaha kama njia pekee ya kujilinda na kudai haki zao. Mmoja wao ni Bore Adugna, ambaye anasema alijiunga na mapambano baada ya kupoteza imani na njia za amani.
“Katika historia ya falme, hakuna taifa lolote ambalo limepata uhuru wake kupitia njia za amani… nilikuja kuamini kuwa suluhisho pekee la dhuluma hii linapatikana kupitia nguvu ya silaha.”
Wachambuzi wanasema mashambulizi ya hivi karibuni ya serikali yamedhoofisha uwezo wa OLA, lakini wanatahadharisha kuwa ukosefu wa usalama, utekaji nyara na makundi ya kihalifu vinaendelea kuifanya Oromia kuwa eneo hatari.
Wakati serikali ikisema hali inaimarika, mashirika ya haki za binadamu yanaonya kuwa mgogoro huu unaendelea bila uangalizi wa kutosha, na raia bado ndio wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wa vita.