Tangazo hilo linaashiria mabadiliko makubwa kwa Rais mwanamageuzi Masoud Pezeshkian, ambaye kwa wiki kadhaa alikuwa ameonya kwamba machafuko nchini mwake yalikuwa yamepita uwezo wake wa kuyadhibiti.
Pezeshkian amesema kupitia mtandao wa X kwamba amemuagiza Abbas Araghchi kufanya mazungumzo hayo kwa kuongozwa na misingi ya utu, busara, na uthabiti, lakini kwa kuzingatia mazingira yanayofaa, yasiyokuwa na vitisho na matarajio yasiyo na msingi.
Marekani bado haijathibitisha ikiwa mazungumzo hayo yatafanyika. Lakini Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Bunge la Mashauriano la Iran Alaeddin Boroujerdi, ameweka wazi mipaka ya nchi yake katika mazungumzo na Marekani, akisema kwamba Iran haina mpango wa kulegeza msimamo juu ya haki zake za msingi na halali. Katika mahojiano na Kituo cha utangazaji cha China CGTN, Boroujerdi alielezea haki ya Iran ya kurutubisha urani kama haki ya msingi.
“Hatutakubali shinikizo kwa kisingizio kwamba Marekani inataka kuwepo katika eneo letu kwa sababu ya rasilimali zetu za mafuta na gesi. Makubaliano ya nyuklia yalikuwa matokeo ya muafaka, ambapo Iran ilikubali ukomo fulani katika urutubishaji urani. Vizuizi katika baadhi ya maeneo vinaweza kujadiliwa, kwa sababu hatutafuti chochote kilicho nje ya haki zetu. Hata hivyo, kuinyima Iran haki ya kurutubisha urani ni kuvuka mipaka.”
Uturuki imekuwa ikifanya jitihada za nyuma ya pazia za kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika baadae wiki hii wakati mjumbe maalum wa Marekani Mashariki ya Kati Steve Witkoff akisafiri kuelekea kanda hiyo. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Oman, Pakistan, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pia wamealikwa kushiriki mazungumzo hayo ikiwa yatafanyika.
Usiku wa jana jumatatu, kituo kimoja cha Al Mayadeen, ambacho kina uhusiano wa kisiasa na kundi la wanamgambo wa Lebanon linaloungwa mkono na Iran, Hezbollah, kilirusha mahojiano na mshauri mwandamizi wa Khamenei kuhusu masuala ya usalama Ali Shamkhani.
Shamkhani, ambaye anaongoza Baraza Kuu la Usalama la Taifa na ambaye aliwahi kuongoza jeshi la majini alipendekeza kwamba iwapo mazungumzo yangefanyika, yangeanza kwa njia isiyo ya moja kwa moja, na kisha baadaye kufuatiwa na mazungumzo ya ana kwa ana endapo kutakuwa na mwelekeo wa makubaliano. Aliongeza kwamba mazungumzo hayo kwa kiasi kikubwa yatatuama katika masuala ya nyuklia.
Katika hatua nyingine, asasi moja isiyokuwa ya kiserikali imesema kwamba mamlaka za Iran zimewakamata zaidi ya watu 50,000 kama sehemu ya hatua zake za kukabiliana na maandamano, ikiongeza kwamba ukamataji huo bado unaendelea. Makundi ya haki za binadamu yamevishutumu vikosi vya usalama kwa kuwaua watu katika ukandamizaji dhidi ya maandamano yaliyoanza Januari 8 na 9 na tangu wakati huo kusambaa.
