Utawala wa Rais Donal Trump wa Marekani umekuwa ukifuatiilia sera ya “mazungumzo na vitisho” kwa wakati mmoja dhidi ya Iran.

Katika suala hili, Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth, akizingatia kauli zinazokinzana za maafisa wa nchi yake, hasa Donald Trump, kuhusu Iran, amekariiri madai kwamba Rais wa Marekani hataki kuingia katika mgogoro na Iran.

Hegseth amedai kwamba: “Rais Trump amejitolea kwa amani na ikiwa Iran ina nia ya dhati kuhusu makubaliano, pia amejitolea kufikia makubaliano. Sasa tunapaswa kuona kitakachotokea.” Akirudia madai ya Washington kuhusu Iran, alidai: “Rais Trump ameweka wazi tangu mwanzo, kama alivyosema kabla ya Operesheni ya Midnight Hammer, kwamba Iran haipaswi kufikia uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia, kwa hivyo ama wajadiliane kuhusiana na hili au tuna chaguzi zingine, na ndiyo maana Idara ya Vita ipo.”

Rais wa Marekani Donald Trump pia alisema katika Ikulu ya White House Jumatatu: “Tunafanya mazungumzo na Iran; tutaona jinsi mambo yatakavyokuwa mwishowe.” Aliongeza, akirudia kauli zake zinazokinzana: “Tumetuma meli kubwa kuelekea Iran na tunafanya mazungumzo na Iran na tutaona jinsi mambo yatakavyokuwa.” Trump alidai: “Tunafanya mazungumzo na Iran na ikiwa tutaweza kufikia makubaliano, hilo litakuwa jambo zuri; na ikiwa hatutaweza, mambo mabaya yanaweza kutokea.”

Katika muhula wa pili wa urais wa Donald Trump, sera ya Marekani ya pande mbili kuelekea Iran imeonekana zaidi. Sera hii ni mchanganyiko wa vitisho vya kijeshi na shinikizo la kiuchumi kwa upande mmoja na mwaliko wa kujadiliana kwa upande mwingine, bila shaka, kwa lengo la Washington kufikia malengo inayotaka kutoka Tehran. Hivyo, inaonekana kwamba tishio la kijeshi na upanuzi wa vikwazo vya kiuchumi hufanya kazi kama njia ya kuifanya Iran ikubali masharti ya Marekani katika mazungumzo yoyote.

Marekani imeiwekea Iran vikwazo vya kila upande na inataka mazungumzo pasi na kuondoa vikwazo hivyo

Mojawapo ya sababu kuu za sera ya “mazungumzo na vitisho kwa wakati mmoja” dhidi ya Iran chini ya Trump ni wasiwasi unaodaiwa kuhusu uwezo wa Iran wa kuimarisha mpango wake wa nyuklia pamoja na ushawishi wake wa kikanda. Trump amekuwa mpinzani mkubwa wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na alijiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mnamo 2018. Kujiondoa katika makubaliano hayo na kuweka tena vikwazo kulileta aina ya tishio la kiuchumi na kisiasa kwa Iran. Trump aliamini kwamba, kutumia mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa kunaweza kuilazimisha Iran kuketi katika meza ya mazungumzo mpya na kukubali masharti magumu zaidi.

 Kwa upande mwingine, Trump pia amezungumzia uwezekano wa mazungumzo, licha ya mashinikizo ya kiuchumi na vitisho vya kijeshi, ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa wanajeshi wa Marekani hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi. Hali hii ya kuwa na nyuso mbili iinaonyesha jaribio la Marekani la kuunda hali inayofaa kwa mazungumzo ambapo Iran, chini ya shinikizo, italazimika kukubali masharti mapya. Trump ametangaza kwa nyakati tofauti kwamba yuko tayari kujadiliana na Iran. Mwaliko huu wa kujadiliana kwa kweli ni sehemu ya mkakati wa utawala wa Trump, ambao unalenga kuunda fursa za kufikia makubaliano mapya na magumu zaidi yenye madai zaidi kutoka Iran. Mbali na madai ya nyuklia, yaani kufikisha urutubishaji madini ya urani katika kiwango sifuri na kuharibifu au kuondolewa akiba ya kilo 400 ya urani iliyorutubishwa kwa 60%, Trump sasa anataka kuweka vikwazo vikali kwa uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, pamoja na mabadiliko ya msingi katika sera ya kikanda ya Tehran kwa kuacha kusaidia mhimili wa muqawama katika eneo.

Sababu nyingine ya sera hii, hasa katika muhula wa pili wa Trump, ni mabadiliko katika milingano ya kikanda na kimataifa. Trump anatafuta kukabiliana na ushawishi wa Iran katika eneo la Asia Magharibi, na katika suala hili, anataka kuizuia Tehran kuunga mkono makundi ya muqawama Asia Magharibi kwa kutumia shinikizo la kiuchumi na kisiasa na, katika hatua hii, kutishia kushambulia kijeshi Iran. Katika suala hili, Marekani inajaribu kuilazimisha Iran kubadilisha tabia na sera zake kupitia vitisho vya kijeshi na kuimarisha vikwazo, hasa kwa kuweka vikwazo vikubwa kwa mauzo ya nje ya mafuta.

Trump amekuwa mpinzani mkubwa wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na alijiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mnamo 2018.

Matokeo ya sera hii ya nuso mbili kuhusu Iran yamekuwa makubwa, hasa katika uwanja wa mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na usalama. Kwa upande mmoja, shinikizo na vikwazo vya kiuchumi vilivyoanza mwaka wa 2018 kama sehemu ya sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Trump vimepunguza mapato ya mafuta ya Iran na kuongeza matatizo yake ya kiuchumi. Lengo la Trump limekuwa kuivua na kuongeza hali ya kutoridhika ndani ya Iran, kuongeza mashinikizo kwa watu wa Iran, na kuunda machafuko ya ndani nchini Iran. Bila shaka, Tehran imejibu shinikizo hizi kwa kuimarisha na kupanua mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani, kuendelea na majaribio ya makombora, na kuongeza uwezo wake wa ulinzi.

Kwa upande mwingine, mwaliko wa Trump wa mazungumzo umeifanya Iran kufuatilia kwa karibu hali na mazingira, na wakati mwingine kupunguza mvutano, kutangaza utayari wake wa kujadiliana na Marekani, ingawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Hata hivyo, baada ya raundi tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani mwaka wa 2025, huku Tehran ikitarajia raundi ya sita ya mazungumzo, Trump, ndani ya mfumo wa sera ya udanganyifu, wakati huo huo aliupa utawala wa Kizayuni ruhusa ya kushambulia Iran, na Washington hata ilikuwa na nafasi ya moja kwa moja katika uvamizi huu wa kijeshi kwa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran kwa mabomu.

Kwa sasa, Trump na maafisa wa utawala wake wanaendelea kutekeleza sera hiyo ya hiyo ya “mazungumzo na vitisho kwa wakati mmoja” kwa kupeleka vifaa vya kijeshi Asia Magharibi na wakati huo huo wakitoa wito wa mazungumzo, lakinii, kwa kuzingatia masharti na ajenda ya Washington. Kwa upande mwingine, Iran, huku ikisisitiza haki zake halali, hasa katika uwanja wa shughuli za nyuklia ambazo zinafanyika kwa malengo ya amani, imesisitiza uwezekano wa kujadili suala hili kwa mfumo wa haki na uadilifu, huku ikikataa mazungumzo yoyote kuhusu uwezo wake wa makombora na himaya kwa mhimili wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *