Rais Trump amesema makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, kuahidi kuacha kununua mafuta kutoka Urusi kutokana na vita vya Ukraine vinavyoendelea.

Ikulu ya Marekani, White House imesema ushuru wa ziada wa asilimia 25 uliowekwa mwaka uliopita kutokana na India kununua mafuta ya Urusi, umepunguzwa hadi asilimia 18, hatua inayomaliza miezi kadhaa ya kutokuwa na uhakika.

Trump amesema pia India imekubali kununua bidhaa za Marekani zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 500, ikiwemo nishati, teknolojia, bidhaa za kilimo, makaa ya mawe na bidhaa nyingine. India pia itapunguza ushuru wake wa uagizaji kwa bidhaa za Marekani hadi sifuri.

Mazungumzo yenye tija

Kwa upande wake Modi amesema mazungumzo kwa njia ya simu kati yake na Trump yalikuwa mazuri na amefurahishwa kwamba bidhaa zinazotengezwa India sasa zitapunguzwa ushuru hadi asilimia 18. Modi amemshukuru Trump kwa niaba ya watu bilioni 1.4 wa India kutokana na tangazo hilo.

Kulingana na Modi, pindi mataifa mawili yenye uchumi mkubwa na demokrasia duniani, yanapofanya kazi pamoja, hali hiyo inawanufaisha watu na kufungua fursa kubwa za ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Modi amebainisha kuwa uongozi wa Trump ni muhimu kwa amani, utulivu na ustawi wa kimataifa. Amesema India inaunga mkono kikamilifu juhudi za amani za Trump, na anatarajia kufanya naye kazi kwa karibu ili kuupeleka ushirikiano wao kwenye viwango visivyo vya kawaida.

DW | 2024 | Sekta ya ngua India
Wachambuzi wametahadharisha kuhusu ukosefu wa uwazi katika vipengele kadhaa vya makubaliano Picha: DW

Shirikisho la Wafanyabiashara wa India Wanaouza Bidhaa zao Nje, FIEO wameyaita makubaliano hayo kama ”baba wa mikataba yote”, na kwamba sekta kadhaa zitashuhudia ongezeko la haraka la manunuzi. Mkurugenzi Mkuu wa FIEO, Ajay Sahai amesema hizo ni habari njema.

Sahai ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba wafanyabiashara wa India sasa watakuwa na ushindani sawa ikilinganishwa na wapinzani wao wa kusini mashariki mwa Asia pamoja na Asia ya Kusini. Anasema wapinzani wao katika ukanda huo bidhaa zao kwa kiasi kikubwa ni zaidi ya asilimia 19.

Mmoja wa wafanyabiashara wa India, Akhilesh Pratap Singh ameyapongeza makubaliano hayo muhimu ya kibiashara yaliyofikiwa kati ya India na Marekani.

”Hii ni hatua nzuri kwa nchi zote mbili, na kwa makubaliano ya kibiashara ambayo yamesainiwa, itaongeza mauzo ya ndani na nje, na itakuwa na manufaa kwa raia pia. Huu ni ushindi kwa nchi zote mbili,” alisisitiza Singh.

Wachambuzi watahadharisha kuhusu uwazi

Hata hivyo, wachambuzi wametoa tahadhari kuhusu ukosefu wa uwazi katika vipengele kadhaa vya makubaliano hayo, ikiwemo madai ya Trump kwamba India itafanikiwa kusonga mbele kwa kupunguza ushuru wake kwa bidhaa za Marekani hadi asilimia sifuri.

Biswajit Dhar, mchambuzi wa masuala ya uchumi anasema watafaidika kutokana na makubaliano hayo, lakini ana wasiwasi kwamba kuna picha kubwa zaidi na hiyo ambayo haiko wazi sana.

Wakati huo huo, wabunge wa chama tawala cha India, National Democratic Alliance, NDA, wamempongeza Modi kwa kufikia makubaliano hayo yaliyosaidia kupunguza viwango vya ushuru kwa bidhaa za India kutoka asilimia 50 hadi asilimia 18.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *