Dar es Salaam. Kumekuwa na ushindani wa chini kwa chini kati ya Marioo na Mbosso, ushindani ambao wasanii hao wenyewe ndio wana uchochea kuliko hata mashabiki kama ilivyo kwa baadhi ya wanamuziki wengine.

Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kimuziki kati ya Marioo na Mbosso kuanzia namba za mauzo, chapa, historia na hata mafanikio kwa ujumla ndani ya tasnia kama ifuatavyo.

FAC 03

1. Mbosso amekuwa katika umaarufu wa kimuziki kwa miaka 12 kwa sababu yeye alitoka kupitia wimbo, Ya Moto (2013) wa kundi la Yamoto Band akiwa na Aslay, Enock Bella na Beka Flavour. Kwa Marioo ana miaka saba kwani alitoka na wimbo wake, Dar Kugumu (2018), hiyo ikiwa ni baada ya kufanya jitihada nyingi za kuwaandikia nyimbo wasanii mbalimbali ili kujitambulisha.

2. Mafanikio makubwa ya Mbosso yalikuja baada ya kusainiwa na lebo ya WCB Wasafi, lakini kwa Marioo ni tofauti kwani amevuma bila kuwa chini ya lebo yoyote kitu anachojivunia hadi sasa.

3. Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Marioo ameshinda tuzo nne, huku Mbosso akishinda mbili ambapo moja alishinda akiwa na Yamoto Band 2015, na ya pili akiwa solo chini ya WCB Wasafi 2022.

FAC 01

4. Hata hivyo, Mbosso ndiye wa kwanza kushinda TMA, wakati Marioo alianza kushinda tuzo hizo mwaka 2022, kisha 2023, ambapo kila mwaka aliibuka na ushindi wa tuzo mbili.

5. Video za Mbosso zimetazamwa YouTube zaidi ya mara bilioni 1.0 tangu ajiunge na mtandao huo Novemba 2, 2017, huku Marioo akitazamwa mara milioni 511.1 tangu ajiunge Januari 4, 2018.

6. Na Mbosso ni mwanamuziki wa tano Tanzania kutazamwa YouTube zaidi ya mara bilioni 1 baada ya Diamond Platnumz, Rayvanny na Zuchu. Hii ni rekodi ambayo Marioo ndio kwanza yupo katikati ya safari kuifikia.

FAC 04

7. Marioo ana lebo yake, Bad Nation ambayo imemtambulisha mwanamuziki mmoja, Stans ambaye wameshirikiana katika wimbo, 2025 (2024). Naye Mbosso ana lebo, Khan Music, lakini bado hajamtambulisha msanii yeyote.

8. Marioo ametoa albamu mbili, The Kid You Know (2022) na The God Son (2024), huku zote zikiwa na deluxe, yaani nyongeza ya nyimbo, kolabo au remix ambazo hazikuwepo katika toleo la awali la albamu.

FAC 02

9. Lengo la msanii kufanya deluxe ni kuendeleza mauzo (streams), kuitangaza tena upya albamu baada ya muda fulani na kuongeza thamani  ya kazi ya awali katika soko. Katika albamu ya kwanza (The Kid You Know) nyimbo zilitoka kupitia delux ni; Nikazama, Sing, Tomorrow na Tunamjua. Na katika albamu ya pili (The God Son), nyimbo zilikuja na delux ni; Dunia, Njozi na Oluwa. 

10. Kwa upande wake Mbosso, yeye ana albamu moja, Definition of Love (2021) pamoja na Extended Playlist (EP) mbili, Khan (2022) na Room Number 3 (2025). Albamu yake (Definition of Love) haikufanyiwa delux huku EP ya kwanza (Khan) ikimpatia tuzo ya TMA kama Msanii Bora wa Kiume wa Bongofleva 2022 akiwabwaga Marioo, Harmonize, Dully Sykes na Alikiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *