Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Nandy ameweka wazi namna ambavyo mwimbaji wa nyimbo za injili nchini, Obby Alpha alivyohusika katika uandishi wa wimbo wake mpya unaotamba, ‘Asante’.

Kupitia chapisho la ujio wa albamu ya mwimbaji huyo wa injili, aliloweka katika ukurasa wake wa Instagram, Nandy aliweka ujumbe akimmwagia sifa kwa utunzi bora wa wimbo wa Asante huku akiitabiria makubwa albamu hiyo.

“Kwa uandishi wa asante, album itakuwa noma sana. Mungu akubariki mtumishi” ameandika Nandy katika uwanja wa maoni.

Aidha, mara baada ya Obby kuchapisha ujumbe huo Nandy alirudi tena na kushukuru kwa wimbo huo unaowabariki watu wengi, “Asante sana kwa hit song inabariki watu wengi sana,” ameandika.

Hii sio mara ya kwanza kwa Obby Alpha kuhusika katika uandishi wa nyimbo za injili zilizoimbwa na wasanii wa Bongo Fleva. Utakumbuka Novemba 19, 2023, ulitoka wimbo wa Asante wa Marioo ambao ulikuja baada ya wimbo wa Bora Kushukuru kutoka kwa Obby Alpha uliyotoka Septemba 6, 2023.

Akizungumza na Mwananchi, Obby Alpha amesema japo hakuhusika kwenye uandishi wa wimbo wa Marioo, lakini alitumika kama hamasa baada ya wimbo wake Bora Kushukuru.

“Sijahusika kwenye uandishi wa wimbo wa Marioo, naweza nikasema ilikuwa ni hamasa kutoka kwenye wimbo wa ‘Bora Kushukuru’ uliotoka mwaka 2023. Napenda mtu akiimba nyimbo za shukurani kwasababu Mungu anatuambia tushukuru kwa kila jambo,” amesema Obby

Amesema shauku yake kubwa ni kuona watu tofauti na wasanii wa injili wakiimba nyimbo za gospel kwani husikilizwa zaidi kutokana na ushawishi wao mkubwa.

“Shauku yangu kubwa ni kuona mtu anayeimba nyimbo za kidunia aimbe nyimbo za injili. Unajua watu wanaoimba nyimbo za kidunia wanaushawishi mkubwa sana kwenye jamii. Kwahiyo akifanya kitu cha Kimungu anagusa maisha ya watu wengi zaidi ya watu wa injili wakati mwingine.

“Kwasababu atasikilizwa na watu ambao hata hawaendi kanisani, lakini sisi tunaweza kupata wa kanisani pekee, mfano mzuri ni wimbo wa Asante hata Nandy mwenyewe hakuamini kama utafanya vizuri,” amesema Obby.

Obby Alpha ameweka wazi anatamani kumuona Nandy akiimba nyimbo za injili mara kwa mara kwani anamashabiki wengi wanaomfuatilia makanisani.

“Hata tulivyokuwa studio nimemwambia napenda zaidi akiimba injili. Kwasababu kuna nyimbo kama mbili nimesikia akiimba na kuna watu nimesikia kanisani wanasikiliza nyimbo za Nandy alizoimba gospel,” amesema Obby.

Obby Alpha kwa sasa ameachia albamu yake ya pili inaenda kama Tabasamu iliyotoka Februari 2, 2026, ikiwa na jumla ya nyimbo 20.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *